AMKA NA BWANA LEO 30
KESHA LA ASUBUHI
JUMANNE, MACHI, 30, 2021
SOMO: NITILIE MAFUTA KATIKA TAA YANGU
Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema BWANA wa majeshi.
Zekaria 4:6.
Hatuhitaji kudhani kwamba kwa sababu sisi ni nuru ndogo tu, kwamba hatuhitaji kuwa mahsusi kuhusu kuangaza. Thamani kuu ya nuru yetu hutegemea kutogeuka geuka katika kuangaza katikati ya giza la kimaadili la dunia, katika kuangaza si kwa kujipendeza wenyewe na kujitwalia utukufu kwa ajili yetu wenyewe, bali kumtukuza kwa vyote tulivyonavyo. Ikiwa tunatenda kazi kwa ajili ya Mungu, na kazi yetu inalingana na uwezo Mungu aliotupatia, hiyo ndiyo yote anayotarajia kwetu....
Tunajua kuwa taa zinazotupatia mwanga hazina mwanga katika zenyewe. Haziwezi kujijaza zenyewe. Kwa hiyo watakatifu waliochaguliwa ni lazima wamimine mafuta ya dhahabu katika mabomba ya dhahabu. Na moto wa mbinguni, ukiwekwa, huzifanya ziwake na kuangaza nuru. Mioyo yetu haiwezi kuakisi nuru mpaka kuwe na muunganiko hai na mbingu. Hii pekee inaweza kuwafanya wawake kwa uthabiti kwa upendo mtukufu usio na ubinafsi kwa Yesu, na kwa wote walionunuliwa kwa damu yake. Na ikiwa kwa kudumu hatutajazwa kwa mafuta ya dhahabu, mwale utazimika. Ikiwa upendo wa Mungu si kanuni ya kudumu katika mioyo, nuru yetu itatoweka....
Shetani na malaika washirika wake huwaelekeza wale wanaodai kuwa watoto wa Mungu, lakini ambao kwa tabia na matendo yao huonesha kwamba wanafanana na mwasi, na kumdhihaki Kristo na malaika wa mbinguni. Hata lini tutamsulubisha Mwana wa Mungu upya, kwa hiyo Mungu anaaibishwa kutuita wana na binti zake? Je, si wakati wa sisi kuweka kando mambo ya kitoto? Je, tutakuwa katika idadi ya wale ambao hujifunza muda wote, bali kamwe hawezi kuufikia ufahamu wa kweli?
Ni mafuta ya dhahabu ambayo wajumbe wa kimbingu humimina katika mabomba ya dhahabu, kuchukuliwa kwenda kwenye bakuli ya dhahabu, ndiyo hutengeneza mwanga wa kudumu, unaoangaza vizuri. Ni upendo wa Mungu ambao ukihamishiwa kwa kudumu kwa mawakala wa kibinadamu humdumisha kuwa nuru angavu sana kwa Mungu. Kisha anaweza kuwapatia nuru na kweli kwa wale wote walio katika giza na makosa na dhambi.
Mafuta ya dhahabu hayatengenezwi kwa ujuzi wa kibinadamu. Ni uweza usioonekana wa mjumbe mtakatifu anayesimama mbele za kiti cha enzi cha Mungu kumpatia kila mmoja aliye gizani ili aweze kutawanya nuru ya mbinguni. Katika mioyo ya wale waliounganishwa na Mungu kwa imani, mafuta yake ya dhahabu ya upendo hububujika bure.
Post a Comment