Mafunzo ya watu wazima leo 26
KESHA LA ASUBUHI
IJUMAA, FEBRUARI, 26, 2021
SOMO: SIRI YA UTAKASO
Kwa kuwa Mungu, aliyesema, Nuru itang'aa toka gizani, ndiye aliyeng’aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa Mungu katika uso wa Yesu Kristo.
2 Wakorintho 4:6
Kristo anatuagiza kuangaza kama nuru katika ulimwengu, kwa uakisi nuru ya Mungu kama inavyoonekana katika uso wa Yesu Kristo. Ni nani miongoni mwetu hufanya hili? Je, maisha yetu hung’aa kwa nuru hii ya ajabu? Mungu humtarajia kila mmoja wetu kuiakisi sura yake kwa ulimwengu. Tumeongozwa hatua kwa hatua kusonga mbele. Tumetembea na kufanya kazi kwa imani, na tunahitaji kujitia katika nidhamu binafsi kuvumilia magumu kama askari wazuri wa Yesu Kristo.
Tunataka fikra nzuri, zenye nguvu ambazo hazikatishwi tamaa kwa urahisi, fikra zilizofundishwa kupambana na magumu tutakayokutana nayo, kupambana na kuyashinda matatizo magumu. Ni sharti tuinue kiwango cha kweli katika miji na majiji yanayotuzunguka. Ni lazima tuone kile kinachopaswa kufanyika na kukifanya katika upendo na kicho cha Mungu. Wakati tumeenda mbali kwa kadiri tunavyoweza kwa imani, ndipo Bwana atakapotenda kwa niaba yetu.
Ni Mungu ndiye aliyetutia nguvu kuianza kazi hii. Tumeenda mbele hatua kwa hatua, kwa kuomba, kwa kuamini, tukifanya kazi. Mungu ndiye mwanzilishi wa Imani yetu, na tunakapofanya kila mmoja sehemu yake, huitimiliza kazi, akilitukuza jina lake mwenyewe katika kuitimiliza. Bwana huwatia nguvu watendakazi wake waliojiweka wakfu kufanya si kutoka katika kile wakionacho bali kwa kile Bwana akionacho.
Tunapaswa kuimarisha nafsi zetu kwa tumaini, dada pacha wa imani. Mtenda kazi wa Mungu ni sharti aishi katika utii mkamilifu kwa mapenzi ya Mungu. Kuna hatari ya kufanya kazi kwa makusudi yanayopingana na Mungu, kwa kuwa mwanadamu anataka kufanya njia yake, anayoidhania kuwa ndiyo njia bora kabisa kuyafikia makusudi ya Mungu. Lakini hatuwezi kuwa na njia na nia yetu wenyewe. Ni lazima Mungu atende kazi ndani yetu na kwa kututumia na kupitia kwetu. Tunapaswa kuwa katika mikono ya Mungu kama vile udongo katika mikono ya mfinyanzi, ili aweze kutufinyanga katika mfanano wa kiungu.
Mioyo yetu inahitaji kuwekwa wakfu kikamilifu kwa Mungu. Hebu tusitafute kudumisha njia na nia yetu wenyewe. Mungu ametupatia kweli yake, ili iweze kututakasa, kutusafisha, na kuadilisha utu wetu mkamilifu. “Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu” (1 Wathesalonike 4:3). "Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipaswavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe” (1 Petro 1:3).
Post a Comment