Historia ya wimbo "Kaa Nami"

91-Kaa Nami (AbideWith Me)

Kaa nami, ni usiku tena;
Usiniache gizani, Bwana
Msaada wako haukomi;
Nilipeke yangu, kaa nami.

Siku zetu hazikawii kwisha;
Sioni la kunifurahisha;
Hakuna ambacho hakikomi,
Usiye na mwisho kaa nami.

Nina haja nawe kila saa:
Sina mwingine wa kunifaa
Mimi nitaongozwa na nani 
Ila wewe? Bwana kaa nami.

Sichi neno uwapo karibu;
Nipatalo lolote, si taabu; 
Kifo na kaburi haviumi;
Nitashinda kwako, kaa nami.

Nilalapo nikuone wewe,
Gizani mwote nimulikiwe;
Nuru za mbinguni hazikomi, 
siku zangu zote; kaa nami.

*Historia ya wimbo no 91*

Wimbo huu upendwao kuimbwa na wengi hususani nyakati za usiku ulitungwa na mchungaji Henly Francis Lyte (1793-1847). Aliutunga wimbo huu mnamo mwaka 1847 kabla ya kufariki kwake, akiwa na kumbukumbu ya msiba wa rafiki yake mpendwa aliyefariki miaka michache mwanzoni mwa utumishi wake, pamoja na fungu la Luka 24:29 lisemalo, “Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao”.
Kumbukumbu zinaonesha kuwa, mchungaji Henly alisumbuliwa na ugonjwa wa Pumu (Athma) na mwishoni mwa maisha yake alipata maambukizi ya TB (Tuberculosis). Hali yake ilipozidi kuwa mbaya, aliamua kuhamia kusini mwa Ufaransa akitumaini kuwa hali ya joto iliyopo huko ingemsaidia kupunguza changamoto za maumivu. Lakini pamoja na kuhamia Ufaransa, aliendelea kudhoofu siku baada ya siku. Kwa mara ya mwisho aliposimama kuhubiri, alikuwa dhaifu sana kiasi kwamba alishindwa kuhitimisha somo lake, ikabidi asaidiwe. Jioni ya siku hiyo, aliamua kuandika  wimbo huu “kaa nami”, ukielezea juu ya masumbufu ya hapa ulimwenguni na uhusiano wa dhati na Yesu kristo; akauambatanisha na tuni yake, kisha akawapatia ndugu zake.  Haikupita muda mrefu, Henly alifariki dunia. Wimbo wake ulidumu kwa muda murefu; na mnamo mwaka 1867, tuni mpya ilitungwa na William Henry Monk.
William Henry Monk alizaliwa tarehe 16, mwezi wa 3, mwaka 1823, huko London-Uingereza. Alianza kupewa kazi ya Uchezaji kinanda kanisani akiwa na umri wa miaka 18. Alitumika kwenye makanisa manne ya London kama mcheza kinanda, na mnamo mwaka 1849, alichaguliwa katika chuo cha “King’s college” kuwa kiongozi wa kwaya. Ilipofika mwaka 1874, aliteuliwa kuwa muhadhiri wa muziki katika chuo hicho cha “King’s college”. Na mwaka 1882 alitunukiwa shahada ya muziki (D.Mus.) kutoka katika chuo kikuu cha Durnham. Sambamba na hayo, Willium pia alikuwa ni muhariri wa maswala ya Muziki.
Maisha yake yote aliyoyaishi, alithamini sana muziki; na mawazo yake yalijawa na uchezaji wa kinanda kwa lengo la kumtukuza Mungu, si maburudisho na maonyesho. 
Historia ya kutungwa kwa tuni hii tunayoitumia sasa inaeleza kuwa, Wiliam H. Monk (ambaye pia alikuwa ni muhariri) alikuwa na kikao pamoja na Muhariri mwenza(Sir Henry Baker) kilichofanyika kwake(Willium). Walipokuwa wamemaliza kikao na kuanza kutawanyika, walikumbuka kuwa walipaswa kutengeneza tuni mpya ya wimbo huu wa “Kaa nami”. Ndipo waliporudi ndani, na Willium pasipo kuchanganywa na kelele za wanafunzi wengine waliokuwa chumba jirani wakijifunza uchezaji wa kinanda, alitumia dakika 10 kukamilisha tuni ya wimbo huu “Kaa nami” ambayo inatumika hadi hivi leo.

*Somo katika wimbo namba 91*

Historia iliwahi kutolewa ya tajiri mmoja, aliyekuwa ni mfanya biashara mahiri mwenye mafanikio makubwa. Alikuwa na mke pamoja na mtoto wa kike mmoja tu, na wote kwapamoja walikuwa ni wacha Mungu.Siku moja akiwa safarini kuelekea kwenye biashara zake, alipata ajali iliyosababishwa na kupasuka kwa tairi ya mbele ya gari lake alilokuwa akisafiria, kisha kupinduka. Gari la tajiri huyo ilibondeka vibaya sana. Raia walipokuja kutazama, walimkuta tajiri akiwa amekatika miguu pamoja na mikono yake yote, kisha wakamkimbiza hospitalini kwa ajili ya matibabu na baadae alirudishwa nyumbani kuendelea kuhudumiwa na mke wake.
Baada ya muda kupita, mke wa tajiri huyo alipokea taarifa ya mwaliko ikimtaka ahudhurie kwenye harusi ya kaka yake. Alishauriana na mume wake aliyekuwa tayari-kilema na mume wake akaridhia mwaliko huo.Siku husika ilipofika, alihakikisha amemuhudumia mume wake vizuri, na kuweka kila kitu vizuri, kisha akaagana naye na kuanza safari kuelekea harusini akiwa pamoja na binti yake.

Baada ya sherehe kuisha, mke wa tajiri alianza safari kurudi nyumbani akiwa na binti yake ndani ya gari lao. Wakiwa njiani, kwa bahati mbaya gari lao lilipata ajali iliyotokana na kugongana na Roli lililokuwa limekosa muelekeo, na wote kwapamoja (mama na mtoto) wakafariki palepale.Watu walipofika kwenye eneo la tukio, walisikitishwa sana kwa ajali ile. Wengi walijiuliza, “ni kwa namna gani, na ninani ampelekee tajiri- kilema tarifa?” Kijana mmoja aliamua kuchukua jukumu hilo. Baada ya huyu tajiri kupata tarifa, alitazama juu huku machozi yakimtiririka kisha akasema kama Henly F. Lyte kuwa, “ Tafadhali Bwana, nipo peke yangu, kaa nami.”

 “Na Mimi nitakaa kati ya wana wa Israeli, nami nitakuwa Mungu wao.” (Kutoka 29:45)

Kitendo cha Mungu kuwatoa wana wa Israeli Misri na kuwapeleka Kanani, kilionyesha nia ya kuwa nao na kuwalinda. Walipoanza safari, Mungu aliwatangulia kwa mfumo wa wingu nyakati za mchana na nguzo ya moto nyakati za usiku.Walipofika jagwani, Mungu alizidi kuwa karibu nao zaidi kwa kuamua kuishi katikati yao (  kutoka 25:8).Hii inadhihirisha wazi kuwa, Mungu wetu anampenda mwanadamu kuliko kawaida, anapenda kukaa naye,kuzungumza naye, na hata kula pamoja naye (Ufunuo 3:20; Isaya 1:18). Biblia inadhihirisha wazi kuwa sisi tu mali ya Mungu, lakini lazima tukumbuke kuwa uamuzi wa kumkaribisha akae nasi upo mikononi mwetu. Mpendwa, mruhusu Mungu akae nawe; Usithubutu kamwe kumuacha akapita kando katika maisha yako, mruhusu atawale kila kitu ulichonacho, utaona baraka tele hata katika changamoto.
Mtunzi wa wimbo huu baada ya kupitia changamoto za magonjwa, anaandika akisema, “Bwana usiniache gizani”.
 Giza analolizungumzia si giza la usiku, bali ni giza la huzuni, mashaka, magonjwa, maumivu makali, kukoswa msaada, na matatizo mengi yaliyo mazito katika maisha haya; akijua kuwa, hakuna mwingine awezaye kumfariji na kumpa msaada, isipokuwa Mungu peke yake. Pia anaonyesha kuwa, katika shida zake, hakuna aliyeweza kumpatia furaha na kumuongoza kufikia hali nzuri isipokuwa Mungu peke yake.

Mpendwa msomaji, Mungu anapokaa nasi, hakuna mlima wowote katika maisha yetu utakaotubabaisha; Mungu akikaa kati yetu, msaada wake utakuwa thabiti katika maisha yetu na hatutakuwa na upweke kamwe. Yeye akikaa nasi, magonjwa, misiba, kuonewa na matatizo mengine mengi yatupatayo, kamwe hayatatufedhehesha maana tumaini letu litakuwa lipo kwake, na mikononi mwake tutakuwa salama. Hebu ombi langu na lako liwe, “kaa nami Bwana.”

1 comment:

  1. Kaa nami ni usiku... Wimbo mzuri na historian take inagusa moyo

    ReplyDelete