amka na Bwana
KESHA LA ASUBUHI
Jumanne 18/08/2020
*KUJIOKOA MIMI MWENYEWE KWA KUWAOKOA WENGINE*
*Jitunze nafsi yako, na mafunndisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia.* 1Timotheo 4:16
📜 Nimesoma juu ya mtu fulani ambaye, alipokuwa akisafiri siku moja ya msimu wa baridi kupitia katika mikondo yenye kina ya theluji, akatiwa ganzi kwa baridi, ambayo bila kutambua ilikuwa inagandisha nguvu zake za lazima kwa uhai. Alikaribia kufa kwa kuzizima-kupata baridi kali kupita kiasi, na alikuwa karibu kuachana na jitihada za kuendelea kuishi, aliposikia vilio vya msafiri mwenzake ambaye pia alikuwa anaangamia kwa baridi.
📜 Huruma yake iliamshwa, naye akadhamiria kumwokoa. Aliisugua miguu baridi ya mtu huyu mwenye bahati mbaya, na baada ya juhudi kubwa za kutosha akamwinua asimame kwa miguu yake. Yule mwenye shida aliposhindwa kusimama, alimbeba kwa mikono yenye huruma kupitia katika mikondo ile ile ambayo alifikiri kuwa asingeliweza kuipita peke yake.
📜 Alipokuwa amembeba msafiri mwenzake hadi kwenye mahali pa usalama, ukweli ulimjia ghafla akilini kwamba katika kumwokoa jirani yake alikuwa pia amejiokoa. Juhudi zake za dhati za kumsaidia mwingine zilihuisha damu ambayo ilikuwa inaganda katika mishipa yake yeye mwenyewe na kupeleka joto lenye kutia afya katika mikono na miguu yake.
📜 Somo kwamba katika kuwasaidia wengine sisi wenyewe tunapokea msaada lazima lihimizwe kwa waumini vijana kila wakati, kwa kanuni na kwa kuonesha mfano, ili kwamba katika uzoefu wao wa Kikristo waweza kupata matokeo bora kabisa. Hebu wale wanaokata tamaa, wale wanaoelekea kufikiri kuwa njia ya kuelekea katika uzima wa milele ni yenye kujaribu na ngumu, waende kazini kwa ajili ya kuwasaidia wengine.
🔘 *Juhudi kama hizo, zikiunganishwa na maombi kwa ajili ya kupata nuru kutoka kwa Mungu, zitasababisha mioyo yao wenyewe kupigapiga kwa uwezo unaohuisha wa neema ya Mungu, upendo wao uking 'aa zaidi kwa ari takatifu. Maisha yao yote ya Kikristo yatakuwa halisi zaidi, yenye ari zaidi, yaliyojaa maombi zaidi… Shuhuda wanazozibeba katika huduma za Sabato zitajazwa na nguvu. Kwa furaha watashuhudia uzuri wa uzoefu ambao wameupata katika kufanya kazi kwa ajili ya watu wengine.*
*MUNGU AKUBARIKI SANA*👮♂️
Post a Comment