UTAAHIRA ktk Mahusiano ya karne HII

NENO LA LEO - HUU NAO NI UTAAHIRA KATIKA MAHUSIANO
 
Kizazi Chetu kinazidi kukumbwa na Ugonjwa Mbaya wa kupungukiwa na akili (UTAAHIRA) hasa katika eneo la kuanzisha Mahusiano ya Uchumba na hatimaye NDOA. 

Sikiliza neno linasema - "Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na BWANA." Mithali 19:14.

Hebu tutafakari; Hii mitindo ya Kuonjana kwanza Kama unaonja Maparachichi na hatimaye kuacha Kama sio zuri, au kuanza Kukaa pamoja ili Kujuana na hatimaye kuhalalisha ndoa au kuachana, au mitindo ya Kurukiana Kama Panzi na kuanzisha maisha, au kuwapanga Kama Maembe halafu unachagua - Je hapo BWANA Anahusishwa? HUO NDIO UTAAHIRA.

Majeraha mengi, Machungu mengi na Vilio vingi vinavyoendelea katika Ndoa za leo na Katika Mahusiano ni matokeo ya hii hali ya UTAAHIRA. Ndio neno linasema - "Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake." Mithali 6:32.

Jambo la kushangaza zaidi ni pale unaposikia hata wanaojiita Vijana wa Yesu, au Watumishi, Wana wa NURU nao wanadai hawawezi kuuziwa Mbuzi kwenye Gunia, ni Bwana yupi wanayemtumikia? ni Yule Mungu wa akina Yusufu, Kweli ni Yule wa Danieli, yule wa akina Isaka? Ni Kweli Vijana wote wa kike na wa Kiume katika Kizazi hiki ni MATAAHIRA? 

Zingatia; Uwe ulianza vibaya na unapitia Machungu, uwe uko kwenye mchakato wa Mahusiano yasiyo na mwelekeo, uwe katika ndoa iliyo ndoano, uwe katika hali yoyote isiyo na matumaini - BADO LIPO TUMAINI. Simama kwa Ujasiri mtazame BWANA, anajua Pambano ulilonalo, naye yupo Kukusaidia, atakusamehe na kukupatia tumaini Jipya.

NAWATAKIA TAFAKARI NJEMA NA MIANZO YENYE MATUMAINI MAPYA.

Na: Ev. Eliezer Mwangosi

No comments