amka na Bwana

Kesha La Asubuhi, Mei 27

Moyo Uliochangamka ni Dawa Nzuri

Moyo uliochangamka ni dawa nzuri; Bali roho iliyopondeka huikausha mifupa.
Mithali 17 : 22.

Uhusiano uliopo baina ya akili na mwili ni wa karibu mno. Moja inapoumizwa, nyingine husononeka. Hali ya akili huathiri afya kwa kiasi kikubwa kuliko tunavyoelewa. Magonjwa mengi yawakabiliyo wanadamu leo ni matokeo ya fadhaa kiakili. Huzuni, wasiwasi, kutoridhika, hasira, hatia, kutokuamini, yote hudhoofisha nguvu za uhai, na kuleta uchakavu na kifo.

Ugonjwa unaletwa, na kuendelezwa zaidi, kupitia mawazo yetu. Wengi ni dhaifu maishani mwao mwote ambao wangalikuwa wazima endapo wangaliwaza hivyo. Ujasiri, tumaini, imani, huruma, upendo husaidia kuleta afya na maisha marefu. Akili tulivu iliyoridhika, roho yenye uchangamfu, ni afya kwa mwili na nguvu kwa roho. Shukurani, uchangamfu, ukarimu, kutumainia upendo na ulinzi wa Mungu—hizi ni kinga bora za afya.

Nguvu ya nia na umuhimu wa kujitawala nafsi, yote katika uhifadhi na urejeshaji wa afya, fadhaa na uangamivu utokanao na hasira, kulalamika, uchoyo au unajisi, na kwa upande mwingine, nguvu tele ya ajabu itokanayo na tabasamu, ukarimu, shukurani, vyapaswa kuoneshwa.

Upo ukweli kisaikolojia—ukweli ambao twapaswa kuutambua—katika Maandiko, "Moyo uliochangamka ni dawa nzuri" Mithali 17 : 22 Kanuni za kweli za Ukristo hutufungulia milango ya furaha isiyo na kifani. Twapaswa kuhimiza uchangamfu, tumaini na amani akilini mwetu, kwani afya yetu hutegemea utulivu wa kiakili.

No comments