Advertisement

Responsive Advertisement

SHULE ZA MISINGI KONGWE KUKARABATIWA NA SERIKALI

Pamoja na Serikali kuendelea kutoa elimu bure kuanzia Darasa la kwanza hadi kidato cha Nne ,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tamisemi Ummy Mwalimu amesema Serikali ina mpango wa kukarabati Shule za Msingi Kongwe zilizojengwa kabla ya Uhuru ili kuzirudisha kwenye hadhi yake ya Awali .

Waziri Ummy akizungumza Mjini Bagamoyo wakati akikabidhiwa Madarasa saba ya Shule ya Msingi Kaole, yaliyokarabatiwa na Taasisi ya Billal Muslim Mission of Tanzania kwa Ufadhili wa Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Lady Fatemah Trust (UK). Amesema.

"Pamoja na Mipango mingine tuliyonayo ya kuboresha elimu Msingi na Sekondari pia Serikali tumedhamiria kukarabati Madarasa na Majengo mengine ya shule zetu za Msingi kongwe ili wanafunzi wanaosoma sasa waone fahari ya kusoma kwenye shule hizo. Tumeanza kukarabati Shule kongwe za Sekondari ambazo zitakamilika mwaka huu, mwakani tunageukia Shule Kongwe za Msingi" alieleza Waziri Ummy.

Waziri Ummy, amewashukuru Lady Fatemah UK na Billal Muslim Mission of Tanzania kwa msaada wao wa Takribani Shillingi milioni 70 katika kufanya ukarabati huu hapa katika shule ya Msingi Kaole.

Sambamba na Ukarabati wa Vyumba saba vya Madarasa pia Taasisi ya Lady Fatemah Trust (UK) imekarabati Ofisi ya Mkuu wa Shule,Ofisi ya Walimu na kujenga matundu 2 ya Vyoo vya walimu.

Aidha katika hatua nyingine Waziri Ummy ametoa rai kwa wadau wengine wa Maendeleo kujitokeza kuunga mkono Mpango wa ukarabati wa Shule Kongwe zilizojengwa kabla na miaka ya mwanzoni baada ya Uhuru ili kufanikisha kuwa na mandhari mazuri ya Usomaji na Ufundishaji kwa watoto wetu.

Post a Comment

0 Comments