SERIKALI KUIMARISHA MIUNDOMBINU YA BANDARI

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuboresha miundombinu ya bandari ili kuvutia idadi kubwa ya watumiaji zikiwemo nchi za ukanda wa Maziwa Makuu.

Ameyasema hayo leo (Jumanne, Julai 20, 2021) alipokutana na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Leonard Chamuriho, Mkurugenzi wa Bandari, TASAC, TBS, TMDA, Kamishna wa Forodha pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya usafirishaji.

Amesema lengo la kikao hicho ni kufanya tathmini ya hatua zilizofikiwa katika uboreshwaji wa huduma mbalimbali bandarini zikiwemo za upakuaji wa mizigo.

Waziri Mkuu amesema Serikali imejipanga kununua vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mizigo yote inayopitia bandarini inapakuliwa katika kipindi cha muda mfupi.

Amesema bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga zimefanyiwa maboresho makubwa, hivyo amewasisitiza wadau wa sekta binafsi waendelee kuleta meli za kutosha.

Waziri Mkuu amesema mbali na maboresho yaliyofanyika katika bandari hizo, pia bandari za Kabwe, Kasanga nazo zimeboreshwa pamoja na ujenzi wa bandari ya Karema ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria katika nchi za Congo, Zambia na Burundi.

Naye, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Chamuriho amesema kuwa ujenzi ndani ya bandari ya Dar es Salaama unaelekeka kukamilika “Gati zote saba tumezimaliza na sasa tunamalizia eneo la makontena katika gati namba sita na saba ambalo litakamilika mwezi Agosti, 2021, hii itasaidia kuongeza ufanisi ndani ya bandari”

No comments