RAIS HUSSEIN MWINYI AUPONGEZA UTAYARI WA TONY BLAIR

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza utayari wa Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Tony Blair wa kuiunga mkono Zanzibar kupitia taasisi yake ya  Mabadiliko Ulimwenguni (Tony Blair Institute for Global Change).
 
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mstaafu  huyo wa Uingereza Tony Blair ambaye  alikuwepo Zanzibar kwa ziara maalum ya siku moja.
 
Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana na Taasisi ya Waziri Mkuu huyo Mstaafu wa Uingereza ili kuihakikisha azma iliyokusudiwa inafikiwa.
 
Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri huyo Mstaafu wa Uingerza kwa kufanya ziara Zanzibar na kuweza kubanilishana mawazo katika mustakbali mzima wa kuiletea maendeleo Zanzibar.
 
Alieleza kwamba ana matumaini makubwa kuwa mazungumzo baina yao yatakuwa chachu ya maendeleo hasa ikizingatiwa kwamba Tony Blair ni kiongozi wmenye mwenye uzoefu mkubwa wa uongozi duniani.
 
Hivyo Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani zake kwa Waziri Mkuu huyo Mstafu na kueleza kwamba nia yake njema ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Taasisi yake ya Mabadiliko Ulimwenguni (Tony Blair Institute for Global Change) itaweza kuleta manufaa makubwa ya kimaendeleo.
 
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Waziri Mkuu huyo juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane katika kutekeleza mikakati, mipango  na dira zilizowekwa na Serikali ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kuiletea Zanzibar maendeleo endelevu

No comments