NDUMBARO ATOA SIKU 21 KWA TAWA KUPITIA UPYA KANUNI

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro ametoa muda wa takribani  wiki tatu kuanzia leo kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), kuzipitia upya kanuni zinazowezesha watu binafsi kuanzisha na kumiliki mashamba ya wanyamapori.

Dkt. Ndumbaro ametoa muda huo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro wakati akizungumza na wamiliki wenye mashamba yenye  wanyamapori Kanda ya Kaskazini,  kwa lengo la kujadili changamoto za uendeshaji na umiliki wa mashamba hayo.

Amesema wametambua urasimu uliopo kwenye utoaji wa leseni kwa watu binafsi wanaotaka kuanzisha na kumiliki mashamba ya  Wanyamapori,  hivyo kurekebishwa kwa kanuni hizo kutasaidia kuondoa  vikwazo kwa watu hao. 

Dkt. Ndumbaro pia ameitaka TAWA kuendelea kuyafanyia kazi maombi ya leseni za watu binafsi wanaotaka kuanzisha na kumiliki mashamba yenye Wanyamapori yaliyopokelewa haraka  iwezekanavyo,  kwani bila kufanya  hivyo Wawezekaji watapotea.

Kwa upande wao baadhi ya wamiliki wa mashamba yenye Wanyamapori wamesema kauli ya Waziri wa Maliasili na Utalii  imewapa muelekeo mpya kwa kuwa kanuni zilizopo kwa sasa haziwasaidii katika kufuga  wanyamapori kwenye mashamba yao.

No comments