CHUO CHA UALIMU TARIME KUBORESHWA

Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika vyuo vya ualimu nchini ikiwemo Chuo cha Ualimu Tarime ambacho baadhi ya miundombinu yake ni ya muda mrefu.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga alipotembelea Chuo hicho ili kujionea maendeleo ya uboreshaji wa miundombinu ambapo amesema lengo la Wizara ni kuboresha miundombinu ili walimu tarajali wasome katika mazingira mazuri na wezeshi ili watoke wakiwa na weledi.

Katika ziara hiyo walimu tarajali hao wamemweleza Mhe. Kipanga changamoto zinazowakabili kwa sasa ikiwemo kukosekana uzio pamoja na uchakavu wa mabweni ya wavulana ambapo Mhe. Kipanga ameahidi kuwa Wizara itazishughulikia

“Tumepokea changamoto zenu, tunazichukua na tunaahidi kama Wizara kuzifanyia kazi ,” amesema Mhe. Kipanga.

Awali Mkuu wa Chuo cha Ualimu Tarime, Roman Urassa alimweleza Naibu Waziri Kipanga kuwa katika mwaka wa fedha 2017/2018 Chuo kilipokea fedha kiasi cha Shilingi bilioni 1.19 kutoka katika Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) kwa ajili ya kujenga na kukarabati baadhi ya miundombinu ya chuo huku mwaka 2019/20 kikipokea gari jipya aina ya Toyota Land Cruiser Hard Top ambalo pia lilinunuliwa na Mradi huo.

No comments