Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amezindua mradi wa usambazaji wa umeme wa ‘Peri Urban’ jijini Dodoma ambao utakamilisha usambazaji wa umeme katika maeneo yote yaliyokuwa yamesalia kufikiwa na nishati hiyo muhimu.
Akizindua mradi huo jana, Waziri Kalemani amesema mradi huo umegharimu kiasi cha Sh bilioni 17.3 ambapo umelenga kusambaza umeme katika kwenye maeneo yote ambayo hayajafikiwa katika mitaa 222 ya jijini humo.
“Kupitia mradi huu wa umeme, mtaunganishiwa kwa Sh 27,000 kama nilivyosema awali na imani yangu ni kwamba utachochea shughuli za uchumi na kijamii hivyo niwaombe sana muitumie vizuri fursa hii ambayo Mh Rais Mama Samia Suluhu Hassan ametutaka tutekeleze mara moja ili tuwaondolee adha wananchi kwa kukosa umeme.
“Kwa hivyo basi na mimi namuagiza Mkandarasi Cylex kutoka Sri Lanka kuanza utekelezaji mara moja ili baada ya mwezi mmoja na nusu nije niwashe mwenyewe hapa,” amesema Waziri Kalemani.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Antony Mtaka amewataka wananchi wote kuhakikisha wanaitumia nishati hiyo kama kichocheo cha kujiletea maendeleo na hasa kwenye kuongeza ufaulu kwa watoto wa shule ambao watapata muda mrefu wa kujisomea katika mazingira rafiki kuliko ilivyokuwa awali.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Mhe. Anthony Mvunde aliishukuru serikali chini ya Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya usambazaji wa umeme ya Peri Urban na Densification ambayo kukamilika kwake kutaliwasha Jiji lote la Dodoma na hivyo wananchi kutumia nishati hiyo kujiletea maendeleo mbali mbali hasa katika sekta za kiuchumi.
0 Comments