Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Prof. Abel Makubi ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kuongoza katika matibabu ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao (njiti) hapa nchini.
Prof. Makubi amesema hayo leo alipokua akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mh. Kassim Majaliwa katika mbio maalumu za Bima Marathoni za kuwezesha upatikanaji wa Tzs. 100 mil. ambazo zitatumika kununua vifaa tiba kwa ajili ya kuwahudumia watoto njiti. Mbio hizo zilianzia katika viwanja vya Mlimani City, Dar es Salaam na zilikuwa za kilometa tano, kumi na 21.
Amebainisha kwamba asilimia 13 hadi 17 ya watoto wanaozaliwa hapa nchini ni njiti hivyo wanahitaji uangalizi maalumu ili waweze kukua vizuri.
"Watoto hawa huathiriwa pia na magonjwa ya maambukizi ya bakteria au kushindwa kupumua baada ya kuzaliwa na kuchangia asilimia 80 ya vifo vyote vya watoto wachanga na kuongeza kuwa dozi moja ni Tzs. 600,000" amesema Prof. Makubi.
Pia, Prof. Makubi ametumia fursa hiyo kuwashauri Watanzania kukata bima na kujenga mazoea ya kufanya mazoezi ili kuwa na afya bora.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu amekabidhi mfano wa hundi ya Tzs. 100 mil. kutoka kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya kununua vifaa vya matibabu ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao (njiti).
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga & Mloganzila, Prof. Lawrence Museru amesema Muhimbili inapokea watoto njiti 20 kila siku idadi ambayo inajumuisha wanaozaliwa Hospitali ya Muhimbili na wanaozaliwa katika Mkoa wa Dar es Salaam na Hospitali za rufaa nchini.
Amesema kutokana na hali hiyo imeilazimu hospitali kuongeza wodi za watoto wachanga, kuboresha huduma za watoto wachanga mahututi kwa kuanzisha ICU ya watoto wachanga ( Neonatal ICU) yenye vitanda saba na vitanda 13 vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu sanjari na kuwapatia mafunzo wahudumu wa afya ili waweze kukidhi mahitaji ya wodi hiyo.
0 Comments