CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeshiriki ibada ya kuaga mwili wa Profesa Mwesiga Baregu, iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Usharika wa Kunduchi Beach, Dar es Salaam.
"Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amemtaja Profesa Mwesiga Baregu kuwa alikuwa ni mwanazuoni mzalendo, aliyetumia taaluma yake katika kuimarisha na kuhuisha demokrasia nchini
"Pia ni mwanasiasa nguli aliyependa siasa safi na siasa za hoja kwa ustawi wa watanzania, daima tutamkumbuka na kuenzi." amesema Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, wakati akiwasilisha salamu za rambirambi kwa niaba ya Chama.
Msemaji wa familia hiyo Profesa Kaijage, amemshukuru Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Samia kwa moyo wake wa kiungwana, kwa kuwa nao katika kipindi chote cha msiba na maombelezo ya mpendwa wao.
"Rais Samia ametufariji sana, wote mlisikia kupitia Vyombo vya Habari na mitandao baada msiba huu kutokea alitufariji, kwa salamu za pole na leo amemtuma mwakilishi wake ametupa nguvu na tunathamini sana hili kwa kuwa tumekuwa nae katika kipindi hiki kigumu kwetu wanafamilia," amesema Profesa Kaijage.
Mwili wa Profesa Baregu umesafirishwa kwenda nyumbani kwao, Mkoani Kagera kwa Maziko.
0 Comments