Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Ummy Mwalimu ameagiza kuanzia Julai Mosi mwaka Huu, kuanza uhakiki wa tiketi za kielektroniki katika usafiri wa mabasi yaendayo kwa haraka kwa kutumia mfumo wa POSS ili kudhibiti upotevu wa mapato
Waziri Ummy amesema hayo leo wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Hassani Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhusu kuboreshwa kwa usafiri huo
Amesema kuwa utekelezaji wa hilo ni hatua za awali wakati unasubiriwa mfumo mkubwa utakaohuisha matumizi ya kadi na mageti ambao ndio utakaokuwa ni suluhu ya kudumu.
Waziri Ummy ametaka uhakiki huo wa kutumia poss kuanza haraka wakati mfumo mkubwa unaotarajiwa kutekelezwa Novemba mwaka huu, unasubiriwa ili kuepuka udanganyifu, wizi na upotevu wa mapato.
"Nataka mapema tuwe tumekomesha utoaji wa tiketi zisizohakikiwa, hapa tunaruhusu wizi kufanywa watu wanakuwa na vitabu vyao vya tiketi, Rais Samia na Waziri Mkuu waliyasema haya," amesema Waziri Ummy
Ameendelea kusema kuwa matumizi ya tiketi hizo kunapelekea kujitokeza kwa udanganyifu na wizi wa mapato kutokana na baadhi ya watendaji wasio waaminifu kuingiza sokoni tiketi zao na kusisitiza kuwa lazima kuwepo kwa utaratibu unaohakikisha tiketi zinatolewa moja kwa moja katika mashine na kumfikia abiria wakati huo.
Amesema kuna changamoto nyingi zinazotokana na utoaji wa huduma katika mabasi yaendayo kasi ambazo kimsingi zinapaswa kutatuliwa kwa lengo la kumuondolea usumbufu mwananchi huku ikibainika kuwepo kwa hali kila upande kutotimiza majukumu yake kikamilifu.
Waziri Ummy amewaagiza watendaji wa Wakala wa mabasi yaendayo haraka ( DART) pamoja na mtoa huduma wa mabasi hayo (UDART) kukutana Dodoma katika kikao kitakachofanyika kesho ili kutafuta suluhisho la changamoto ya mabasi hayo Jijini Dar-es-salaam.
0 Comments