Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 23 Mei, 2021 ameshiriki kwa njia ya mtandao mkutano wa mtandao wa viongozi wanawake Barani Afrika (AWLN) ulioitishwa na Rais Mstaafu wa Liberia Mhe. Ellen Johnson Sirleaf kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa uongozi na kupeana
taarifa juu ya fursa mbalimbali.
Viongozi wengine walioshiriki mkutano huo ni Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ethiopia Mhe. Sahle-Work Zewde, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mhe. Amina Mohamed, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Malawi Mhe. Joyce Banda na Rais Mstaafu wa Serikali ya Mpito ya Jamhuri ya Afrika Kati Mhe. Catherine Samba-Panza.
Wengine ni Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Mauritius Mhe. Ameena Gurib-Fakim, Mwanzilishi wa AWIN Tanzania na Katibu Mkuu wa Mkutano wa Nne wa
Wanawake Duniani Mhe. Getrude Mongella, Mjumbe Maalum wa Afrika katika masuala ya amani na usalama Mhe. Dkt. Bineta Diop na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya wanawake Bi. Phumzile Mlambo-Ngeuka.
Viongozi hao wamempongeza Mhe. Rais Samia kwa kupokea kijiti cha Urais, na wamemuahidi ushirikiano wowote atakaouhitaji katika uongozi wake katika masuala mbalimbali yakiwemo maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii, haki za wanawake, amani na usalama wa kikanda na janga la ugonjwa wa Korona (Covid-19.).
Katika majadiliano hayo, viongozi hawa wamemueleza Mhe. Rais Samia fursa mbalimbali zilizopo katika mashirika na taasisi kimataifa ambazo zinatoa ufadhili wa fedha, teknolojia na ujuzi kwa ajili ya maendeleo ya nchi mbalimbali duniani na wamemshauri kutumia fursa hizo ili kutimiza malengo yake ya kuiongoza Tanzania.
Mhe. Rais Mstaafu Ellen Sirleaf amesema wana matumaini makubwa na Mhe. Rais Samia na kwamba wanawake wa Afrika wanamtegemea kuwa msemaji wao na mfano wa kuigwa.
Mhe. Getrude Mongella ameelezea kufurahishwa kwake na kutimin kwa ndoto yake ya miaka mingi ambapo alitamani kuona Tanzania inakuwa na Rais Mwanamke na kwamba yupo tayari kuwahamasisha wanawake wote wa Tanzania
kumuunga mkono Mhe. Rais Samia ili aongoze kwa mafanikio makubwa.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Samia amewashukuru viongozi hao kwa majadiliano
waliyoyafanya na ushauri walioutoa kwake na amewaahidi kuwa yupo tayari kushirikiana nao na kushirikiana na taasisi na mashirika mbalimbali ya kimataifa katika kufanikisha jukumu la kuipeleka mbele Tanzania.
Ameahidi kuendelea kuwapa nafasi za uongozi wanawake wengi zaidi katika Serikali anayoiongoza ili kufikia lengo la 50 kwa 50, kuimarisha upatikanaji wa huduma za kijamii zikiwemo afya, maji, elimu na miundombinu kama
inavyoelekezwa katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka 5 na kuendelea kupunguza vifo vya akina mama wakati wa kujifungua.
Juhudi nyingine ni kukabiliana na changamoto za mazingira ambazo zinapunguza mvua na uzalishaji wa mazao, kuweka uwazi katika matumizi ya fedha za umma na kuongeza juhudi za kukabiliana na Covid-19, hivyo ametoa wito kwa washirika mbalimbali maendeleo kuongeza ushirikiano na Tanzania.
Mhe. Rais Samia amewaomba viongozi hao kuendelea kujadiliana na kubadilishana mawazo mara kwa mara juu ya kulisaidia Bara la Afrika kupiga hatua za kimaendeleo na kuinua zaidi ustawi wa jamii hasa wanawake na watoto ambao
wanakabiliw na madhara changamoto nyingi.
0 Comments