Advertisement

Responsive Advertisement

MAAFISA HABARI WATAKIWA KUZINGATIA MIONGOZO

Katibu Mkuu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amewataka Maafisa Habari,Mawasiliano na Uhusiano kote nchini kuzingatia maelekezo, mbalimbali ya viongozi wakuu na miongozo inayotolewa na Serikali wakati wanapoandaa mikakati ya mawasiliano kwenye maeneo yao.

Dkt Abbasi ambaye ni mtaalam mbobezi kwenye taaluma ya Habari ametoa kauli hiyo Mei 25, 2021 wakati akichangia uzoefu wake kwenye mada ya Uandaaji wa Mkakati wa Mawasiliano na utekelezaji wake” iliyowasilishwa na mwanahabari mkongwe, Innocent Mungy kwenye kikao kazi cha Maafisa Habari,Mawasiliano na Uhusiano (TAGCO) kinachoendelea Jijini Mbeya.

Amesema Serikali imekuwa na maelekezo mahususi ya kimkakati ambayo ni muhimu kuyaingiza ili kuleta matokeo bora wakati wa kufanya tathmini ya utendaji wa kazi za taasisi za Serikali.

Akiwasilisha mada hiyo Mungy amesisitiza kuwa mkakati wa mawasiliano ni nyenzo muhimu inayosaidia taasisi kufanya kazi kwenye kiwango kinachopimika.

Mwenyekiti wa kikao kazi hicho ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Ally Possi alitaka ufafanuzi wa namna gani Maafisa Habari wanaweza wakawafanya baadhi ya viongozi wasiopenda na kutambua umuhimu wa kuwa na mikakati ya mawasiliano kwenye maeneo yao ambapo ilielezwa kuwa ni kwa kuwashirikisha.

Naye Dkt. Peter Mataba wakati akiwasilisha mada ya “Mkakati wa Mawasiliano” amesisitiza kuwa taasisi zinapaswa kuzingatia ujumbe unaopelekwa kwa hadhira, na malengo ya taasisi husika ambayo yanatekelezeka kulingana na Mpango Mkakati wa taasisi husika.

Post a Comment

0 Comments