Advertisement

Responsive Advertisement

TAGCO YAMPA TUZO DKT. ABBAS

Katibu Mkuu wa Habari wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi ametunukiwa tuzo na Chama cha Maafisa Habari na Mawasiliano wa Serikali (TAGCO) kwa kutambua mchango na mageuzi makubwa aliyoyafanya kwenye Sekta ya Habari hapa nchini.

Akikabidhi tuzo hiyo kwa Dkt. Hassan Abbasi, Mwenyekiti wa TAGCO, Paschal Shelutete wakati wa kikao cha 16 cha chama hicho kilichofanyika Jijini Mbeya Mei 24, 2021 amesema Dkt. Abbasi ametoa mchango mkubwa akiwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Mkuu wa Serikali tofauti na hapo awali.

“Ni katika kipindi hiki ambapo miradi ya kimkakati ya Serikali ilisemewa vizuri zaidi na kufahamika na watu wengi hivyo kuwafanya wananchi kuipenda Serikali yao” Amefafanua Shelutete.

Ameongeza kwamba Dkt. Abbasi amefanikiwa kusimamia tasnia ya Habari na uboresha mahusiano ya kikazi miongoni mwa wadau wote wa Sekta ya Habari.

Kwa upande wake Dkt. Abbasi amewashukuru Maafisa hao kwa kumpa tuzo hiyo na kuahidi kuendelea kuwapa ushirikiano ili waweze kuendelea kutekeleza majukumu wao kikamilifu kwa nafasi yake ya sasa ya Katibu Mkuu. Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo.

“Tuendelee kushirikiana katika cheo hiki kipya cha Katibu Mkuu katika Wizara yetu ambayo ni Wizara muhimu inayogusa umma kwa nyanja ya burudani na huzuni kutokana na Sekta zake” ameongeza Dkt. Abbasi.

Amewataka maafisa hao kuzingatia weledi wakati wote wa uandaaji wa kazi ambapo amesisitiza kwamba Serikali inatambua mchango wa maafisa habari na kwamba itaendelea kuhakikisha sekta inaboreka na kuchangia kwenye uchumi wa Taifa.

Aidha amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumwamini na kumrejesha tena kwenye nafasi ya Katibu Mkuu na kuahidi kufanya kazi kwa weledi na bidi ili kutekelea Ilani ya Chama cha Mapinduzi na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia.

Kikao hicho kimefunguliwa na Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Innocent Bashungwa na kimehudhuriwa na Naibu wa Wizara hiyo, Pauline Gekul, Katibu Mkuu -TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe.

Post a Comment

0 Comments