Waraka wa Pasaka nchini Tz kufutwa na serikali

SERIKALI imeliandikia barua Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ikilitaka kuufuta waraka wa Pasaka uliotolewa Machi mwaka huu vinginevyo hatua kali za sheria zitachukuliwa dhidi ya kanisa hilo.

Waraka huo uliopewa jina la ‘Taifa letu amani yetu’ ulisainiwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo.

Ulijikita kujadili masuala ya jamii, uchumi, siasa, katiba mpya na matukio ambayo yako kinyume na kile lilichokiita tunu na misingi ya Taifa.

Jana, Mtanzania ilimtafuta Kiongozi wa Kanisa hilo, Askofu Dk. William Shoo kwa njia ya simu kuzungumzia barua hiyo ya serikali lakini hakupatikana.

Pia Mtanzania lilifika ofisi za makao makuu ya KKKT mjini Arusha kuonana na katibu mkuu wa kanisa hilo ambaye hakuweza kupatikana.

Katibu muhtasi wake alisema kiongozi huyo alikuwa nje ya ofisi akihudhuria vikao nje ya ofisi.

Mwandishi aliacha mawasiliano yake ofisini hapo baada ya kushauriwa kuacha namba yake ya simu ili apigiwe baadaye baada ya kiongozi huyo kutoka kwenye vikao.

Hata hivyo hadi gazeti linakwenda mtamboni jana usiku hakuna simu yoyote iliyopigwa kwa mwandishi kutoka makao makuu ya kanisa hilo.

Alipotafutwa, mmoja wa maaskofu waliosaini waraka huo ambaye ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dk. Stephen Munga, alisema hajapata taarifa yoyote kama kuna barua yoyote kutoka serikalini ikizungumzia waraka huo.

No comments