utulivu KKKT wahitajika wakisubiri majibu ya Mungu
ASKOFU wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa amelitaka Kanisa hilo kutulia na kuona majibu ya Mungu, kwa kuwa nyumba hiyo ndiyo kitovu cha upatanisho na kioo cha upendo na amani katika jamii na siyo vinginevyo.
Aidha, amesema umoja, amani, upendo na utulivu miongoni mwa viongozi na waumini wa dini hiyo, ndiyo kitu pekee kinachopaswa kufanywa kwa sasa ili kuleta maendeleo ya kiroho na kijamii kama ilivyoagizwa na kiongozi huyo. Askofu Malasusa ameyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa ufunguzi na kuweka wakfu Kanisa la Kiinjili na Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Jimbo la Magharibi, Usharika wa Kimara.
Katika uzinduzi huo ulioendana na ufunguzi wa Hospitali ya nyota tano, kituo cha kulea watoto yatima pamoja na shule ya awali na msingi, Askofu Malasusa aliwataka maaskofu, wachungaji pamoja na viongozi wote wa Kanisa hilo kutumia nafasi zao kusambaza upendo wa Yesu katika jamii.“Kanisa ni mahali panapofaa kuonyesha amani hasa kwa nyakati hizi ambapo kumekuwa na dhana mbalimbali, linapaswa kumsikiliza Yesu anasema nini..lipo kwa ajili ya kumhubiri Kristo kwa unyenyekevu..kazi zingine tunazitafuta wenyewe, baadae Mungu atatuuliza,” alisema Askofu Malasusa.
Alisema Kanisa limepewa fursa adhimu ya kuwafundisha na kuwaekeleza watu uzuri wa Yesu hivyo linapaswa kuwa chachu ya amani na upendo kwa kuwa na watu wanaomwamini Mungu wakati wote. Alisema kama ilivyo kwa vitu vingine, Kanisa pia lipo la aina mbili, lile linaloonekana ambalo watu wake wapo kwa ajili ya kuabudu wakiwa na roho ya kweli ya kumuomba Mungu na jingine lisiloonekana ambalo watu wake wanaingia kanisani kwa mazoea. “Natamani kila muumini awepo katika Kanisa linalomwamini Mungu,” aliongeza Askofu Malasusa.
Aidha, Askofu Malasusa aliwapongeza waumini wa Kanisa hilo kwa kufanikisha ujenzi wa Kanisa hilo, Hospitali, Kituo cha kulelea watoto yatima na shule ya msingi na awali kwa kuwa vyote vimelenga kuunga mkono juhudi za kimaendeleo. Awali, Mchungaji wa Kanisa hilo, Wilbroad Mastali, mbali na kumshukuru Askofu Malasusa kwa kushiriki nao katika ibada na ufunguzi wa Kanisa na miradi yake mingine, alisema hatua zinazofanywa na Kanisa hilo zimelenga kuunga mkono jitihada za Serikali kuleta maendeleo hapa nchini. Aidha, aliwataka waumini wote wa dini hiyo kuendeleza ushirikiano wakati wote kwa kuwa ndiyo mambo aliyoyagiza Mungu kwa waumini wake
Post a Comment