Fahamu zaidi kuhusu Patakatifu Pa Patakatifu(Pa Mbinguni)





PATAKATIFU PA MFANO (TYPE) NA PA ASILIA (ANTITYPE)
 JENGO LENYEWE
 Mungu akasema: "NAO NA WANIFANYIE PATAKATIFU; ILI NIPATE KUKAA
KATI YAO." Kutoka 25:8. Hivyo ndivyo alivyoagiza Mungu kujenga jengo ambalo
lingekuwa maskani Yake miongoni mwa wana wa Israeli, na hatimaye kuwa mahali pao
pakuu pa ibada kwa mamia ya miaka. Sio tu Mungu aliamuru lijengwe, bali alitoa mfano
(pattern) wa kufuata katika kulijenga.
 Jengo hili, pamoja na hekalu lililochukua mahali pake [baadaye], lilikuwa ni jengo
lililofurahia sifa ya pekee ya kuwa jengo la pekee duniani ambalo lilipata kufananishwa
na jengo lililoko mbinguni. Kwa mwonekano wake lilifanana na hema. Lilikuwa na
urefu wa karibu futi hamsini na nne, na upana wa futi kumi na nane, na kimo cha futi
kumi na nane. Patakatifu (the sanctuary) palikuwa ni jengo la kupendeza. Vifuniko vya
paa lake vilikuwa vinne. Kuanzia [kifuniko cha] nje, kuelekea kwenye hewa, palikuwa na
ngozi za pomboo. Chini yake ngozi za kondoo waume, zilizotiwa rangi nyekundu. Kisha
chini yake palikuwa na pazia jeupe la singa za mbuzi. Kifuniko cha ndani, ambacho
kiliweza kuonekana kwa makuhani waliohudumu humo, kilikuwa kimetengenezwa kwa
"nguo ya kitani nzuri ya kusokota, pamoja na nyuzi za rangi ya samawi, na ya zambarau,
na nyekundu, pamoja na makerubi, kazi ya fundi stadi." Kutoka 26:l.
 Mbao zenye kusimama, za pande zote mbili na upande mmoja wa jengo lile, zilifunikwa
kwa dhahabu. Mlango wa kuingilia, ambao daima ulikuwa upande wa mashariki,
ulitegemezwa kwa nguzo tano zilizofunikwa kwa dhahabu, ambazo kwazo pazia
lilitundikwa likiwa linaning'inia na hilo ndilo lililofanya "mlango wa Hema, wa nyuzi za
rangi ya samawi, na za rangi ya zambarau, na za rangi nyekundu, na kitani nzuri yenye
kusokotwa, kazi ya mshona taraza." Kutoka 26:36.
 Kulizunguka hema hilo ulikuwa ni ua, futi tisini kwa futi mia moja themanini, ambao
ulizuia wadadisi wasiweze kuangaza macho yao ndani ili kuliona jengo hilo, wala
kuruhusu wale wasiojali kulikaribia jengo hilo kwa karibu sana. Ua huo ulitengenezwa
kwa mapazia meupe ya kitani yaliyoangikwa kwenye vigingi vya shaba vyenye urefu wa
futi tisa. Mlango wake, pia, ulielekea upande wa mashariki, nao ulifungwa kwa pazia
lililofanana na lile la Patakatifu.
 Jengo hili takatifu lenyewe liligawanywa katika vyumba viwili kwa pazia lililotundikwa
kwenye vigingi vinne. Chumba cha kwanza kiliitwa PATAKATIFU, na cha pili,
PATAKATIFU PA PATAKATIFU. Katika chumba kile [cha kwanza] cha Patakatifu
palikuwa na kinara cha taa saba, na meza pamoja na mikate yake ya "wonyesho"
iliyokuwa inabadilishwa mara kwa mara. Zaidi ya [vifaa] hivyo, madhabahu ya
kufukizia uvumba ilisimama mbele tu karibu na pazia la pili [la ndani]. Juu ya
madhabahu hii uvumba wenye harufu nzuri, ukiwa ni mfano wa kazi ya maombezi yake
Kristo inayoendelea [mbinguni] pasipo kukoma, ulifukizwa asubuhi na jioni.

Ndani ya pazia lile la ndani palikuwa ni pale Patakatifu pa Patakatifu, lilimokuwamo
sanduku lenye mbao mbili za Sheria [Amri Kumi], zilizoandikwa kwa kidole cha Mungu.
Kifuniko cha sanduku hilo kilikuwa ndicho kiti cha rehema cha dhahabu. Mwisho wa
kila upande wake alisimama Kerubi mmoja wa dhahabu, mabawa yao yalikutana upande
wa juu, na nyuso zao daima zilikitazama kiti kile cha rehema. Kilikuwa mfano wa kiti
cha enzi cha Mungu ----- malaika wanaokizunguka kiti hicho, sheria ambayo ndiyo
MSINGI WA SERIKALI ya Mungu, na kiti cha rehema chenyewe kilikuwa mfano wa
kuingilia kati kwa rehema na msamaha [wa Mungu] kwa ajili ya mwenye dhambi; na juu
yake utukufu unaoonekana wa Bwana ulikuwapo, yaani Shekina.
 HUDUMA YA UKUHANI
 Fundisho la Biblia kuhusu Patakatifu pa huduma ile ya Walawi huonyesha wazi kwamba
kutakaswa kwa Patakatifu ndilo JIBU LA MUNGU KWA MAKOSA NA UASI.
 Huduma ya ukuhani katika Patakatifu pa Duniani, au Hekalu, katika siku zile za Israeli,
ilikuwa ni mfano wa kazi ya Kristo, Kuhani wetu Mkuu, katika Hekalu la Mbinguni.
Makuhani wa duniani walihudumu kwa "MFANO WA KIVULI CHA MAMBO YA
MBINGUNI." Waebrania 8:5. Na kuhusu huduma yake Kristo katika Hekalu lile la
Mbinguni tunaambiwa hivi:
 "Basi, katika hayo tunayosema, neno lililo kuu ndilo hili TUNAYE KUHANI MKUU
NAMNA HII, ALIYEKETI MKONO WA KUUME WA KITI CHA ENZI CHA UKUU
MBINGUNI, MHUDUMU WA PATAKATIFU, NA WA ILE HEMA YA KWELI,
AMBAYO BWANA ALIIWEKA WALA SI MWANADAMU." Waebrania 8:1,2.
 Katika huduma ya hapa duniani, kutakaswa kwa Patakatifu ilikuwa ni kazi ya Kuhani
Mkuu ya kufungia [mwaka]. Kwa hiyo, kutakaswa kwa Patakatifu wakati ule wa
mwisho, kwa mujibu wa fundisho la hakika la mfano (type), hakuna budi kuwa ni
huduma ya kufungia [kazi] ya Kuhani wetu Mkuu katika Hekalu la Mbinguni, kabla
hajaiweka kando [hajaiacha] kazi Yake ya ukuhani na kuja kwetu katika utukufu wake.
 Palikuwa na sehemu mbili tofauti za huduma ya ukuhani katika Hema kule Israeli.
Kwanza, palikuwa na huduma ya "kila siku," ambayo ilikomea katika chumba kile cha
kwanza. Na sehemu ile ya pili, ni huduma ile ya "kila mwaka," yaani, huduma ya siku ile
ya UPATANISHO, ambayo Kuhani Mkuu peke yake aliruhusiwa kuingia ndani ya
Patakatifu pa Patakatifu.
 H

Kuhusu huduma katika chumba kile cha kwanza inaelezwa hivi: "Basi vitu hivi vikiisha
kutengenezwa hivyo, makuhani huingia katika Hema hiyo ya kwanza daima [kila siku],
wakiyatimiza mambo ya ibada." Waebrania 9:6.
 Kila siku makuhani walihudumu katika chumba cha kwanza. Kila siku walihudumia
"sadaka ya dhambi ya mtu mmoja mmoja," na "sadaka ya kuteketezwa ya daima." Agizo
la Mungu kwa mwenye dhambi mmoja mmoja lilikuwa kama ifuatavyo:
 "Na mtu awaye yote katika watu wa nchi akifanya dhambi, pasipo kukusudia, kwa
kufanya neno lo lote katika hayo ambayo BWANA alizuilia yasifanywe, naye akapata
hatia; akijulishwa hiyo dhambi yake aliyoifanya, ndipo atakapoleta mbuzi mke
mkamilifu, awe matoleo yake kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya. Naye ATAWEKA
MKONO WAKE KICHWANI MWAKE HIYO SADAKA YA DHAMBI, NA
KUMCHINJA SADAKA YA DHAMBI MAHALI HAPO PA SADAKA YA
KUTEKETEZWA. KISHA KUHANI ATATWAA KATIKA HIYO DAMU YAKE
KWA KIDOLE CHAKE, NA KUITIA KATIKA PEMBE ZA MADHABAHU YA
KUTEKETEZA NA DAMU YAKE YOTE ATAIMWAGA CHINI YA
MADHABAHU.... NA
 KUHANI ATAFANYA UPATANISHO KWA AJILI YAKE, NAYE
ATASAMEHEWA." Mambo ya Walawi 4:27-3l.
 Hapa inaonekana picha ya mpango wa Mungu wa kumwondolea dhambi zake yule
mwenye dhambi. Katika nyakati za Agano la Kale kazi hiyo ilitimizwa, kwa mfano, kwa
njia ya damu ile ya sadaka ya dhambi. Katika siku zile mwenye dhambi alileta sadaka
yake, iliyokuwa mfano wa Kristo, penye mlango wa Patakatifu. Pale aliweka mikono
yake juu ya kichwa cha mhanga [kafara] wake asiyekuwa na hatia, naye ilimpasa
KUUNGAMA DHAMBI ZILE ZILE alizokuwa na hatia nazo. Hakutakiwa kusema kwa
jumla tu, bali kutaja dhambi halisi [moja moja kwa jina lake]. Kwa njia ya ibada hii
alizihamishia dhambi zake kwenye kichwa cha mwana kondoo yule.
 Lakini hayo si yote: ilimpasa kwa mkono wake yeye mwenyewe kumchinja mwana
kondoo huyo. Ndipo Kuhani alipoichukua sehemu ya damu hiyo na kuinyunyiza kwenye
pembe za madhabahu ya sadaka za kuteketezwa, na damu iliyobaki aliimwaga yote chini
ya madhabahu hiyo. Kwa njia ya huduma hii yenye madoido mengi dhambi za mwenye
dhambi yule zilihamishwa kwa njia ya damu kutoka kwake kwenda kwenye madhabahu
na hatimaye kufika Patakatifu.
 Kwa njia hiyo "siku kwa siku wanyama wa kafara walichinjwa karibu na madhabahu
mbele ya pazia la nje, na damu 'ililetwa ndani ya Patakatifu' na kuhani." Jambo hili
lilitendeka kukiri UVUNJAJI WA SHERIA ya Mungu [Amri Kumi] na kuwa ushuhuda
kwamba yule mwenye dhambi alistahili kifo. Lilikuwa ni ungamo la imani katikaMwana-Kondoo wa Mungu ambaye angekufa badala ya mwenye dhambi yule, na
ambaye damu Yake ya upatanisho ingemtetea [mwenye dhambi] mbele ya Sheria ya Haki
[iliyovunjwa].
 Siku kwa siku, daima, makuhani walihamisha dhambi kwa mfano (type) kutoka kwa
mwenye dhambi kwenda Patakatifu, na matokeo yake ni kwamba yule mwenye dhambi
alipata msamaha. Tendo hilo lilifanyika aidha kwa kunyunyiza damu "mbele zake
Bwana" au kwa kula sehemu ya nyama ya sadaka ile iliyoteketezwa katika [chumba cha]
Patakatifu.
 SADAKA YA ASUBUHI NA JIONI
 Zaidi ya ile sadaka ya dhambi ilikuwako "sadaka ya asubuhi na jioni," au "sadaka ya
kuteketezwa ya daima." Mungu aliwaagiza watu kwa maneno haya yafuatayo:
 "Basi sadaka utakazozitoa juu ya madhabahu ni hizi; wana-kondoo wa mwaka mmoja
wawili siku baada ya siku daima. Mwana-kondoo mmoja utamchinja asubuhi; na
mwana-kondoo wa pili utamchinja jioni;... Itakuwa ni sadaka ya kuteketezwa milele
katika vizazi vyenu vyote mlangoni pa ile hema ya kukutania mbele ya BWANA; hapo
nitakapokutana nanyi, ili ninene na wewe hapo." Kutoka 29:38,39,42.
 Sadaka ya kuteketezwa ya daima zaidi sana ilikuwa ni sadaka ya taifa zima kuliko kuwa
sadaka ya mtu mmoja mmoja. Ilikuwa ni mfano wa kafara ya Yesu Kristo msalabani, na
mbele za Bwana ilikuwa na harufu nzuri kwa ajili ya Israeli yote. Madhabahu ya sadaka
za kuteketezwa ilikuwa mfano wa msalaba, kama vile kafara juu ya madhabahu hiyo
ilivyokuwa mfano wa kafara ile msalabani. Katika moshi uliopanda juu kutoka kwenye
madhabahu hiyo ulionekana msaada wa kivuli [mfano] wa damu ile iliyomwagika pale
msalabani.
 Sadaka ya asubuhi iliendelea kuteketezwa juu ya madhabahu hiyo mpaka wakati wa
sadaka ya jioni, na sadaka ya jioni iliendelea kuteketezwa mpaka asubuhi. "Hivyo daima
palikuwa na sadaka madhabahuni, mchana na usiku, ishara ya UPATANISHO WA
MILELE uliotolewa
katika Kristo.... 'Sadaka ya asubuhi ilikuwa kwa ajili ya upatanisho wa dhambi
zilizotendwa usiku uliotangulia, sadaka ya mchana [jioni] ilikuwa kwa ajili ya dhambi
zilizotendwa mchana.'" ----- M. L. Andreasen, THE BOOK OF HEBREWS, uk. 372.
 Katika huduma hii kuhani mkuu alinyunyiza damu juu ya kiti cha rehema na Patakatifu;
"kwa sababu ya unajisi wa wana wa Israeli." Patakatifu palisuluhishwa au kutakaswa

kutokana na dhambi zote zilizokuwa zimewekwa pale kwa mfano (type) kwa njia ya
damu ya sadaka iliyoletwa pale siku kwa siku katika kipindi cha mwaka ule.
 Kuhani Mkuu alipotoka nje, akizichukua dhambi, alizihamisha zote kwenda juu ya
kichwa cha mbuzi yule wa Azazeli, ambaye alipelekwa mbali jangwani. Kwa njia hiyo
"dhambi zao zote" zilichukuliwa mbali na kambi lao kwenda jangwani, na Patakatifu
pakawa pametakaswa. (Angalia Mambo ya Walawi l6.)
 Huo ulikuwa ni wakati wa kutisha sana wa hukumu katika Israeli. Maisha ya kila mtu
yalichunguzwa siku ile. Je, kila dhambi ilikuwa imeungamwa? Ye yote ambaye
alionekana hana uhusiano mwema na Mungu, huduma ile ilipoendelea kufanywa,
alikatiliwa mbali [alikufa ghafula] asiwe na sehemu yo yote na watu wake Mungu.
 "Kwa kuwa ni siku ya upatanisho, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu mbele za
BWANA, Mungu wenu. KWA KUWA MTU AWAYE YOTE ASIYEJITESA
MWENYEWE [KWA KUUNGAMA DHAMBI ZAKE KWA DHATI] SIKU IYO
HIYO, ATAKATILIWA MBALI NA WATU WAKE." Mambo ya Walawi 23:28,29.
 SIKU YA UPATANISHO
 Kwa mwaka mzima, isipokuwa siku moja tu, huduma ya ukuhani iliendelea katika
chumba kile cha kwanza, au Patakatifu. Lakini katika siku ile ya mwisho ya huduma ya
mwaka mzima ----- "siku ya kumi ya mwezi wa saba" ----- Kuhani Mkuu aliingia katika
chumba kile cha pili, au Patakatifu pa Patakatifu.
 Katika siku hiyo Kuhani Mkuu alitakiwa kutwaa kutoka mikononi mwa mkutano wa
Waisraeli mbuzi waume wawili. "Kisha [Haruni] atawatwaa wale mbuzi wawili na
kuwaweka mbele za BWANA mlangoni pa hema ya kukutania. Na Haruni atapiga kura
juu ya wale mbuzi wawili; kura moja kwa ajili ya BWANA; na kura ya pili kwa ajili ya
Azazeli. Na Haruni atamleta yule mbuzi aliyeangukiwa na kura kwa ajili ya BWANA, na
kumtoa awe SADAKA YA DHAMBI. Bali yule mbuzi aliyeangukiwa na kura kwa ajili
ya Azazeli ATAWEKWA HAI mbele za BWANA ili kumfanyia upatanisho, ili
kumpeleka jangwani kwa ajili ya Azazeli [Shetani]." Mambo ya Walawi 16:7-10.
 Wakati ule mwenye dhambi alipokuwa ametakaswa kwa damu ile ya sadaka ya dhambi,
wakati alipowekwa huru mbali na dhambi zake na kupatanishwa na Mungu, ilikuwa bado
haijafanyika hatua ya mwisho ya kuziondolea mbali dhambi zake. Zilikuwa
zimehamishwa tu kutoka kwake, kwa njia ya damu ile ya mfano, kwenda Patakatifu. Siku
kwa siku kwa mwaka mzima mamia na maelfu ya wenye toba walileta sadaka zao za
dhambi penye mlango wa Patakatifu, na kwa njia ya damu ya mwana kondoo dhambi zao
zilihamishiwa Patakatifu kutoka kwao.

Siku ile ya Upatanisho [au Hukumu] ilikuwa ni siku ya kilele ya taratibu za kafara
[dhabihu] za mwaka mzima. Katika siku hiyo ondoleo la dhambi la mwisho lilifanyika,
na, japokuwa,
lilifanyika kwa namna ya mfano, hata hivyo, mioyoni mwao lilileta picha, kama vile
linavyoleta picha mioyoni mwetu, ya ondoleo la dhambi la mwisho siku ile ya mwisho.
 "Kisha atamchinja yule mbuzi wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya watu, na kuileta
damu yake ndani ya pazia, na kwa damu hiyo atafanya vile vile kama alivyofanya kwa
damu ya ng'ombe, na kuinyunyiza juu ya kiti cha rehema, na mbele ya kiti cha rehema,
naye ATAFANYA UPATANISHO KWA AJILI YA MAHALI PATAKATIFU, KWA
SABABU YA MAMBO MACHAFU YA WANA WA ISRAELI, NA KWA SABABU
YA MAKOSA YAO, NAAM, KWA AJILI YA DHAMBI ZAO ZOTE.... Wala
hapatakuwa na mtu katika hema ya kukutania, wakati aingiapo ili kufanya upatanisho
katika Patakatifu, hata atakapotoka nje.... Kisha atatoka na kuiendea madhabahu iliyo
mbele za BWANA na kufanya upatanisho kwa ajili yake." Mafungu ya l5-l8.
 KAZI YA KRISTO YA MWISHO MBINGUNI
 Kwa sababu hiyo awamu ya mwisho ya huduma yake Kristo kama Kuhani wetu Mkuu
katika Patakatifu pa Mungu juu, haina budi kuwa kazi ya HUKUMU. Haina budi
kuhusika na kuzichunguza kumbukumbu zile zilizoko mbinguni, sawasawa na huduma
ile ya mwisho katika chumba cha pili katika hema ile ya duniani, yaani, Patakatifu
palipotakaswa.
 Nabii Danieli alionyeshwa badiliko hilo katika huduma ya Kuhani wetu Mkuu, yaani,
kutoka chumba cha kwanza kwenda chumba cha pili katika Hekalu lile la mbinguni.
Anaelezea mandhari hiyo ya ajabu kuwa ni kiti cha Mungu kilicho hai, chenye
magurudumu yake yawakayo moto kwa utukufu Wake, kikiingia katika Patakatifu pa
Patakatifu pale pa mbinguni, kwa madhumuni ya kumaliza kazi ya mwisho ya huduma
yake Kristo:
 "Nikatazama hata viti vya enzi vikawekwa, na Mmoja aliye mzee wa siku ameketi;
mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi;
kiti chake cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao. Mto kama
moto ukatoka ukapita mbele zake; maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi mara elfu
kumi wakasimama mbele zake; HUKUMU IKAWEKWA NA VITABU
VIKAFUNGULIWA." Danieli 7:9,10

Fungu linalofuata linaonyesha kwamba mandhari hii inafunuliwa [hukumu hii
inawekwa] wakati UASI bado unajitukuza wenyewe duniani. Walakini, katika wakati uo
huo HUKUMU INAENDELEA MBINGUNI. Kumalizika kwa kazi hiyo [ya Hukumu]
kutatoa jibu kamili la Mungu kwa uasi huo, na kumfanya Kristo aje mara ya pili katika
utukufu Wake kuja kuukomesha kabisa utawala huo wa dhambi. Ni katika wakati huo wa
kutakaswa kwa Patakatifu ----- wakati ambapo ni kwa hali halisi, sio kwa mfano, kesi
iliyoandikwa Patakatifu inachunguzwa kwa mara ya mwisho mbele zake Mungu. Kazi
hiyo [ya Hukumu] inapofungwa, kulingana na ule mfano [wa Patakatifu pa Duniani], ye
yote ambaye hataonekana kuwa na uhusiano mzuri na Mungu [ambaye atakuwa
hajaungama dhambi zake na kuziacha] atakatiliwa mbali asiwe na sehemu yo yote na
watu Wake waliokombolewa.
 Hapo ndipo huduma ya ukuhani ya Kristo itakapofungwa, na umilele [uzima au mauti]
wa kila mtu utakuwa umefungwa [haubadiliki] kwa milele zote. Hadi wakati ule
utakapofika maneno haya yaliyonenwa na Yesu yatahusika: "MWENYE KUDHULUMU
NA AZIDI KUDHULUMU;... NA MWENYE HAKI NA AZIDI KUFANYA HAKI;
NA MTAKATIFU NA AZIDI KUTAKASWA. TAZAMA, NAJA UPESI, NA UJIRA
WANGU U PAMOJA NAMI, KUMLIPA KILA MTU KAMA KAZI [MATENDO]
YAKE ILIVYO." Ufunuo 22:11,12.
 Lakini kwa wakati huu Mwokozi wetu, toka mahali pake pa huduma huko juu anasema
kwa wote maneno haya ya mausia na matumaini: "Yeye ASHINDAYE [DHAMBI]
atavikwa hivyo MAVAZI MEUPE [HAKI YA KRISTO], wala sitalifuta kamwe jina lake
katika KITABU CHA UZIMA, nami nitalikiri jina lake mbele za Baba yangu, na mbele
ya malaika zake." Ufunuo 3:5.
 Kipindi kile cha unabii cha miaka 2300 kilitolewa ili kuwajulisha watu lini kazi hii ya
hukumu, yaani, kutakaswa kwa Patakatifu, ilianza kule mbinguni. Ni jambo la maana
sana kwetu kujua lini kipindi hicho kinaanza na kumalizika.
-----W. A. Spicer, OUR DAY IN THE LIGHT OF PROPHECY, Sura ya 20, uk.165-
171.
 Type and Antitype (The Sanctuary).
Kwa habari zaidi tafadhali tuandikie: Leaves of Life – International
 S.L.P. 17
 Mafinga Iringa Tanzania

No comments