Padri Anthony Lagwen ameteuliwa kuwa askofu mpya wa jimbo katoliki la Mbulu na Papa Francis.





Mh. Pd. Anthony Lagwen ateuliwa kuwa Askofu Jimbo Katoliki la Mbulu
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Sana Padre Anthony Lagwen kutoka Jimbo Katoliki la Mbulu, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Mbulu, nchini Tanzania. Askofu mteule Anthony Lagwen alizaliwa tarehe 5 Julai 1967 huko Tlawi, Jimboni Mbulu. Baada ya masomo yake ya msingi, alibahatika kuendelea na masomo ya sekondari katika Seminari Ndogo ya Sanu, Jimbo Katoliki la Mbulu. Akapata masomo ya falsafa kutoka Seminari kuu ya Ntungamo, iliyoko Jimbo Katoliki la Bukoba na baadaye akahamia Seminari kuu ya Kipalapala, Jimbo kuu la Tabora ili kuendelea na masomo ya kitaalimungu. Tarehe 18 Oktoba 1999 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre, Jimbo Katoliki Mbulu.
Tangu wakati huo, katika maisha na utume wake wa Kipadre kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2000, alikuwa Paroko-usu wa Parokia ya Bashay. Kati ya mwaka 2000 hadi mwaka 2004 akepelekwa na Jimbo kujiendeleza zaidi katika masuala ya biashara kwenye Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augostino Tanzania, SAUT, Mwanza. Kati ya mwaka 2004 hadi mwaka 2009 akateuliwa kuwa Mchumi wa Jimbo Katoliki la Mbulu. Kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2011 akatumwa tena na Jimbo kujiendeleza zaidi katika masuala ya biashara kwenye Taasisi ya “East and Southern Africa Management Institute” iliyoko Jijini, Arusha. Kuanzia mwaka 2012 hadi kuteuliwa kwake, amekuwa ni mchumi mwaminifu wa mali ya Kanisa, Jimbo Katoliki la Mbulu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Vatican News

No comments