WADAU WA BARUTI NCHINI WATAKIWA KUFUATA SHERIA NA KUUNDA UMOJA

Wadau wa Baruti pamoja na wachimbaji wa Madini nchini wametakiwa kufuata sheria ya Baruti kwenye shughuli za biashara ya baruti na uchimbaji wa madini ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kama vile ajali na kupunguza nguvu kazi ya taifa.

Wito huo umetolewa leo na Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira wa Tume ya Madini, Mhandisi Henry Mditi kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba kwenye mkutano wa wadau wa baruti uliofanyika jijini Dodoma kwa lengo kujadili changamoto zinazojitokeza katika masuala yanayohusu baruti na kutafuta namna bora ya kuzitatua ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kusimamia sheria ya baruti na kanuni zake.

Amesema kuwa serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi, huku masuala ya usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini yakipewa kipaumbele zaidi.

Ameongeza kuwa kuongezeka kwa shughuli za uchimbaji wa madini kumepelekea kuwepo kwa ongezeko la matumizi ya baruti hivyo Serikali kupitia Tume ya Madini imeweka mikakati ya kuzuia ajali za milipuko kwenye migodi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zinazohusu masuala ya baruti zinafuatwa.

Amesema kuwa matumizi ya baruti hapa nchini yameongezeka kutoka wastani wa tani 3,000 kwa mwaka katika miaka ya 1990 hadi kufikia wastani wa tani 32,398 za baruti kwa mwaka 2021 kutokana na ongezeko la shughuli za uchimbaji wa madini, utafiti wa mafuta na gesi asilia na ujenzi wa miundombinu mbalimbali.

"----->Hadi kufikia sasa serikali imesajili jumla ya maghala 253 ya kuhifadhia baruti, na stoo na masanduku 470 ya kutunzia baruti katika migodi mbalimbali na sehemu za biashara, aidha kwa sasa zipo jumla ya kampuni 20 na watu binafsi 10 wanaojihusisha na uuzaji na usambazaji wa baruti hapa nchini"---- Mhandisi Mditi.

Katika hatua nyingine Mhandisi Mditi amesema kuwa Tume ya Madini itaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini kuhusu matumizi sahihi ya baruti ili kuhakikisha wanaendesha shughuli zao kwa kufuata kanuni za usalama.

No comments