MASEJO ATHIBITISHA WATU 5 KUFARIKI KWENYE AJALI ARUSHA

"Ndugu wanahabari leo tarehe 08.09.2021 muda wa saa 10:00 Alfajiri huko Barabara ya Arusha/Moshi eneo la konoike kijiji cha Kolila Tarafa ya king'ori wilaya ya Arumeru Mkoa wa
Arusha kulitokea ajali ambayo ilisababisha vifo vya watu watano na majeruhi mmoja"

"Ajali hiyo ilitokea baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso ambapo gari lenye namba za usajili T.111 CUU aina ya Mitsubish Fuso lililokuwa linaendeshwa na Heriel Jinja (42) Mkazi wa Holili mkoani Kilimanjaro liligongana uso kwa uso na gari lenye namba za usajili T.612 BNN aina ya Mitsubish Canter iliyokuwa ikiendeshwa na Peter Mmasi ambaye bado umri wake na makazi yake hayajafahamika"

"Aidha uchunguzi wa awali umebaini kwamba, chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari aina
ya Mitsubishi Fuso iliyokuwa inatokea Moshi kuelekea Arusha ambapo ilihama upande wa pili
wa Barabara na kugongana na gari aina ya Mitsubish Canter lililokuwa linatokea Arusha kuelekea Moshi"

"Aidha baada ya magari hayo kugongana gari aina Mitsubish Fuso lilipitiliza na kuanguka kwenye mtaro uliopo pembezoni mwa barabara"

"Waliofariki katika ajali hiyo ni Peter Mmasi ambae ni dereva wa gari aina ya Mitsubishi
Canter, Victor Sio Kileo, Vivian Urio na Isack Sio Temba ambao walikuwa abiria wa gari aina Mitsubish Canter na ni wakazi wa Baraa jijini Arusha"

"Aidha katika gari aina ya Mitsubish Fuso aliyefariki ni utingo wa gari hiyo aliyefahamika kwa jina moja Idd mkazi wa Himo mkoani Kilimanjaro"

"Majeruhi katika ajali hiyo ni Heriel Jinja Lymo ambaye amepelekwa katika hospitali ya KCMC Mkoani Kilimanjaro kwa matibabu zaidi na miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya Rufaa ya Mount Meru Jijini Arusha"

"Nitoe wito kwa madereva kuwa makini na matumizi sahihi ya alama za usalama Barabarani ili kuepusha madhara makubwa kwa binadamu ikiwa ni pamoja na kupoteza uhai na uharibifu wa
vyombo vya moto wanavyotumia"-----> Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Justine Masejo.

No comments