RAIS SAMIA AONGEA KWA NJIA YA MTANDAO NA RAIS CHARLES MICHEL

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 12 Julai, 2021 amezungumza kwa njia ya mtandao na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Mhe. Charles Michel.

Mazungumzo hayo yamefanyika Ikulu Jijini Dodoma ambapo viongozi hao wawili wamezungumzia masuala yanayohusu uhusiano kati yanTanzania na Umoja huo.

Mhe. Michel amempongeza Mhe. Rais Samia kwa hatua mbalimbali anazochukua tangu kushika hatamu ya uongozi na kumhakikishia kuwa Umoja wa Ulaya (EU) utaendelea kuwa mshirika muhimu na wa kimkakati wa maendeleo nchini Tanzania na kikanda.

Aidha, Mhe. Michel amempongeza pia kwa jitihada anazochukua kupambana na ugonjwa wa Corona. Vilevile amemueleza kuwa EU tayari inashirikiana na viwanda mbalimbali vinavyozalisha chanjo barani Afrika kwa kuvijengea uwezo na kuongeza kuwa iwapo Tanzania itahitaji msaada huo EU iko tayari kuisaidia.

Kwa upande wake Mhe. Rais Samia ameshukuru Umoja wa Ulaya (EU) kwa ushirikiano katika masuala ya maendeleo ya jamii na kuwekeza
katika miradi ya miundombinu kupitia Benki ya Uwekezaji ya EU. Mhe. Rais Samia amesema kuwa Benki hiyo imetoa Euro milioni 50 kwa ajili
ya ujenzi na ukarabati wa baadhi ya viwanja vya ndege vya mikoani.

Amesema katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita Tanzania na Umoja wa Ulaya zimesaini makubaliano ya msaada wa Euro milioni 111.5 kwa ajili ya kuboresha miradi va sekta ya nishati hususani matumizi ya majiko banifu, uongezaji thamani mazao ya nyuki, kuboresha mazingira ya
biashara na kuimarisha usalama wa chakula.

Mhe. Rais Samia amesema kwa sasa Serikali inaendelea na uboreshaji wa mazingira bora ya uwekezaji kwa sekta binafsi ili kuwezesha
utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) wa Tanzania.

Aidha, Mhe. Rais Samia amemhakikishia Mhe. Michel kuwa utawala wake utasimamia na kuimarisha demokrasia, utawala bora na haki za
msingi za binadamu.

Kuhusu mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona, Mhe. Rais Samia amemtaarifu Rais huyo wa Baraza la Umoja wa Ulaya (EU) Mhe. Michel
kuwa Tanzania tayari imeshajiunga na Mpango wa Kimataifa wa ugawaji wa chanjo kwa nchi masikini (COVAX facility) na ina Mpango wake wa
taifa wa kupambana na Corona unaoainisha mahitaji ya nchi hivyo itawasilisha mahitaji yake kwa EU ili kupata msaada.

Mhe. Rais ameshukuru kupokea mualiko wa kutembelea Umoja wa Ulaya na kumtumia salamu Rais wa Umoja huo Mhe. Bi Ursula von der
Leven.

No comments