PROF. SHEMDOE ATEMBELEA SHULE ILIYOUNGUA MOTO ATTAAUN

KATIBU  Mkuu  Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Prof. Riziki Shemdoe, amefanya ziara ya kutembelea katika Mabweni yaliyoungua na moto shule za Sekondari mbili  ikiwemo shule ya Wasichana ya Kiislamu ya AT-TAAUN na Shule ya Sekondari Charlotte zilizopo Manispaa ya Morogoro.

Ziara hiyo imefanyika jana, Julai 11/ 2020 majira ya asubuhi ya saa 3 akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Albert Msando, Kamati ya ulinzi na usalama, pamoja na Uongozi wa Manispaa ya Morogoro ukiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Pili Kitwana.

Katika ziara hiyo, Prof. Shemdoe, amesikitishwa na uharaibifu wa moto ulioteketeza mali za wanafunzi huku akiwataka waalimu, wanafunzi pamoja na Uongozi wa shule kuwa na subra katika kipindi hiki kifupi  cha mpito.

Prof. Shemdoe, amewaomba Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Zima moto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro washirikiane vyema katika kufanya kutathmini madhara yaliyojitokeza kutokana na moto huo ili Serikali iweze kuwa na taarifa kamili na kujua nini kinaweza kufanyika .

Mwisho, Prof. Shemdoe, amewataka wasimamizi wa Shule kuhakikisha wanafanya maboresho ya mifumo ya umeme mara kwa mara ili kuweza kuzuia majanga kama hayo kutokea

Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Albert Msando  kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Morogoro ,  amemshukuru Prof. Shemdoe kwa ziara yake ya kuwatia matumaini waalimu, wanafunzi pamoja na Uongozi wa Serikali.

DC Msando, amesema kuwa tayari wao kama Viongozi wa  Serikali mara baada ya kupata taarifa ya kuungua kwa mabweni , wamechukua  hatua ikiwemo ya kuhakikisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji  linafika eneo husika na kufanikisha kuuzima moto huo katika shule hizo mbili.

"Tumeona madhara yaliyotokea  katika mabweni ya shule zetu, Jeshi la zimamoto limefanya kazi yake vizuri, nawapa pole sana, lakini kikubwa niwasisitize wasimamizi wa shule waendelee kuchukua tahadhari zote muhimu ili majanga kama haya yasijitokeze tena, naomba sana Uongozi wa Shule husika wawe na subra katika kipindi hiki cha uchunguzi naamini tukishajua chanzo ninini , basi tutawapa taarifa sahihi juu ya nini kinapaswa kufanyika" Amesema DC Msando.

No comments