KUNDO APIGA MARUFUKU MIKATABA KWA LUGHA ZA KIGENI

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesikitishwa na tabia ya baadhi ya watendaji wa makampuni ya simu nchini kuwasainisha wananchi mikataba au makubaliano yeyote ya kutumia ardhi ya mwananchi kujenga mnara kwa lugha za kigeni

Akiwa katika ziara yake ya kukagua ujenzi, uwezo na ubora wa minara ya mawasiliano katika Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga Mhandisi Kundo alitembelea mradi wa ujenzi wa mnara wa Haloteli uliopo katika Kijiji cha Tanga B ambapo baada ya kumhoji mmiliki wa eneo hilo alisema kuwa alisaini mkataba wa makubaliano ya awali ya kufanya ujenzi katika eneo lake uliokuwa kwa lugha ya Kiingereza na kivietinamu

Mhandisi Kundo amepiga marufuku kumsainisha mwananchi mkataba kwa lugha za kigeni kwasababu yeyote anayefanya hivyo lazima kutakuwa na dhamira ovu dhidi ya mwananchi ndio maana anasainishwa mkataba kwa lugha asiyo ifahamu

Aliongeza kuwa, Serikali itasimamia haki na maslahi ya wananchi kwa kuhakikisha wanasainishwa mikataba kwa lugha ya Kiswahili na kiingereza ili pande zote ziweze kunufaika kwa mwananchi kusaini kitu anachokielewa na kulipwa fedha kulingana na ukubwa wa maeneo wanayoyatoa kwa ajili ya ujenzi wa minara ya mawasiliano

Amesema kuwa dhamira ya Wizara hiyo ni kuondoa migogoro ndani ya Sekta ya Mawasiliano kwa watoa huduma kufuata taratibu wakati wa ujenzi wa minara ikiwa ni pamoja na kupata vibali vinavyohitajika na kusaini mikataba na Serikali za vijiji kwa ajili ya ulinzi wa minara ya mawasiliano

Aidha, Mhandisi Kundo alitoa maagizo kwa watoa huduma kufanya malipo kupitia akaunti za benki kutoka kwenye kampuni kwenda moja kwa moja kwa walioingia nao mkataba ambao ni wamiliki wa maeneo waliyojenga minara ili kampuni kujiridhisha inamlipa mhusika na sio vinginevyo

Wananchi wa Kijiji cha Tanga B kilichopo katika Kata ya Kwabada Wilayani Muheza walikiri mbele ya Naibu Waziri huyo kuwa wanahitaji mnara huo wa kampuni ya Halotel ujengwe kwa ajili ya kuwapatia mawasiliano baada ya kampuni hiyo kuhakikisha imefuata taratibu za kupata vibali vinavyohitajika

No comments