TUNATAKA MWANZA IWE KITOVU CHA BIASHARA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 14 Juni, 2021 amekagua ujenzi wa daraja la JPM, amezindua Mradi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira na ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Mwanza - Isaka katika siku ya 2 ya ziara yake Mkoani Mwanza.
Akizungumza na wananchi mara baada ya ukaguzi wa daraja la JPM linalojengwa katika eneo la Kigongo-Busisi, Mhe. Rais Samia amesema ujenzi wa daraja hilo ni sehemu ya mipango ya Serikali ya kulifanya Jiji la Mwanza kuwa kitovu cha biashara kwa nchi za Maziwa.
Mhe. Rais Samia ameiagiza Wizara ya Maji kuhakikisha miradi yote ya maji inatekelezwa kwa wakati ili kufikia lengo la Serikali la kuwaondolea wananchi adha ya upatikanaji wa maji.
Mbali na wito huo, Mhe. Rais pia amewataka wana Misungwi na Watanzania kwa ujumla kuvitunza vyanzo vya maji ili kuendelea kupata majisafi na salama.
Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya Mwanza - Isika yenye urefu wa kilometa 311, utakaogharimu shilingi Trilioni 3.06, amesema mradi huo utaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa kusafirisha kwa haraka na kwa kiwango kikubwa cha mizigo na watu tofauti na ilivyo sasa.
Amesema mradi huu ni sehemu ya mradi mkubwa wa reli kutoka Dar Salaam hadi Mwanza yenye urefu wa kilomita 1,605 ambao utatengeneza ajira 11,000 hivyo kuwataka wana Mwanza kuchangamkia fursa ya ujenzi wa reli hiyo.
Aidha, amesema reli hivo itapunguza muda wa kusafiri kati ya Mwanza hadi Dar es Salaam kutoka saa 17 za sasa kwa usafiri wa mabasi hadi saa 8 mradi utakapokamilika
Post a Comment