SHULE ZATAKIWA KUTENGA MAENEO MAALUM YA MICHEZO

Serikali imeziagiza shule zote nchini kutenga maeneo maalum kwa ajili ya michezo na sanaa ili kuibua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Carolyne Nombo wakati akifungua mashindano ya 41 ya UMISSETA mjini Mtwara, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako, ambapo amesema Wizara ya Elimu itahakikisha kila shule zinakuwa na miundombinu yote muhimu kwa ajili ya michezo ikiwemo michezo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Amesema Wizara itaboresha ufundishaji wa michezo kama vitalu vya vipaji na msingi wa ushiriki endelevu katika michezo kwa afya, elimu, uchumi na ajira.

"Serikali imejizatiti kuendeleza vipaji vya wanafunzi kupitia kufundisha somo la haiba na michezo kwa shule za Msingi, na Elimu kwa Michezo kwa vyuo vya ualimu, pia kupitia wathibiti Ubora wa Shule itahakikisha kunafanyika tathmini na ushauri wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa michezo, elimu kwa michezo na sanaa katika taasisi" amesisitiza Naibu Katibu Mkuu.

Naye Mratibu wa Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA Leonard Thadeo amesema michezo yote iliyoshindaniwa wakati wa mashindano ya UMITASHUMTA itakuwepo kwenyeUMISSETA isipokuwa mchezo wa mpira wa goli ambao haujaanza kushindaniwa katika shule za sekondari.

No comments