SERIKALI KUJENGA KIWANDA CHA KUZALISHA DAWA NCHINI

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa fedha za kujenga kiwanda cha dawa chenye uwezo wa kuzalisha dawa kwa siku mbili ili kuondoa uhaba wa dawa uliopo na kupunguza bajeti ya dawa zinazonunuliwa kutoka nje ya nchi.

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee a Watoto Dkt. Godwin Mollel wakati akiongea na kituo kimoja cha runinga hapa nchini.

Mhe.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameshatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha dawa nchini kitachosaidia kuboresha huduma za afya nchini kwa kuongeza upatikanaji wa hali ya dawa na kupunguza matumizi ya fedha ambazo zingetumika kununua dawa nje ya nchi.

“Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha, sasa kinajengwa kiwanda kule Njombe ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha vidonge maana yake ni kwamba bidhaa za Dawa zitashuka bei, dawa ambayo ilikuwa inanunuliwa mara moja itanunuliwa mara mbili mpaka mara tatu.” Alisema Dkt. Mollel.

Aliendelea kusema kuwa, hali ya huduma za afya inaendelea kuwa bora nchini hususan katika upatikanaji wa dawa, kwani Serikali imeendelea kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya ununuzi wa dawa ili kukabiliana na uhaba uliokuwepo katika kipindi cha nyuma, huku akiweka wazi kuwa, Serikali imeshatoa Bilioni 123 kiasi kilichotoka kabla ya Bajeti ya mwaka huu.

“Kwa kipindi kifupi cha Rais, mama yetu Samia Suluh Hassan alivoingia kwenye Mamlaka, tumepata kiasi cha shilingi Bilion 123 kwaajili ya dawa, hizo ni fedha zilizotoka ndani ya muda mfupi kabla ya hii Bajeti mpya ambayo tumeifanya, ambayo lengo lake ni kwenda kuimarisha suala la Dawa, Vifaa tiba na Vitendanishi.” Amesema Dkt. Mollel.

Kwa upande mwingine amekiri kuwa, Serikali imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusiana na dawa, huku akiweka wazi kuwa tayari Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima ameshapokea mrejesho kutoka kwa timu ya ukaguzi aliyoichagua kwenda katika hospitali za mikoa na utekelezaji wake unaanza kufanyiwa kazi ili kudhibiti mianya yote ya upotevu wa dawa nchini.

No comments