MAJALIWA AZINDUA MPANGO WA TATU WA MAENDELEO NCHINI

Waziri Mkuu Majakiwa Kassim Majaliwa amezindua Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022–2025/2026 utakaogharimu shilingi trilioni 114.8, ambapo sekta binafsi inatarajiwa kuchangia shilingi trilioni 40.6 na sekta ya umma shilingi trilioni 74.2.

“...fedha hizo zinajumuisha mikopo na misaada ya wabia wetu wa maendeleo. Kwa niaba ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kuwahakikishia kwamba fedha hizi zitapatikana na malengo tuliyojiwekea yatatekelezwa.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Juni 29, 2021) wakati akizindua Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022–2025/2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema mpango huo una dhima ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu na umejikita katika kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma; kukuza uwekezaji na biashara; kuchochea maendeleo ya watu; na kuendeleza rasilimali watu.

Amesema Serikali itahakikisha malengo ya Mpango huo yanafikiwa. “Kamwe hatutafumbia macho tabia ya ukwepaji kodi, kazini, ufujaji wa fedha na rushwa na tutaendelea kuenzi bunifu na kupokea mawazo mbadala yenye lengo la kuboresha utekelezaji wa Mpango huu.”

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba amesema mpango huo ni mwendelezo wa jitihada za Serikali za kuimarisha upangaji mipango na kusimamia rasilimali za ndani ya nchi ikijumuisha rasilimali za madini, maliasili, gesi asilia, ardhi, fedha na rasilimali watu kwa lengo la kuboresha hali ya maisha ya Watanzania wote.

Naye, Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Nchini Tanzania, Christine Musisi amesema wananchi, Serikali, wadau wa maendeleo, sekta binafsi watautumia mpango huo kama nyenzo muhimu ya utekelezaji wa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025 na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030. Pia ameihakikishia Serikali kwamba mashirika yote ya Umoja wa Mataifa yataunga mkono utekelezaji wa mpango huo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

No comments