LUKUVI AFUTA WARAKA UNAWAOWABANA MADIWANI
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amefuta waraka namba moja unaowaondoa madiwani kushiriki katika shughuli za uidhinishaji mipango ya uendelezaji miji katika maeneo yao uliotolewa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi nchini.
Kabla ya kutolewa waraka huo mpya Madiwani kupitia kamati zao za mipango miji walikuwa ndiyo wenye mamlaka ya kubariki mipango ya uendelezaji miji katika halmashauri husika kupitia vikao vyao vya robo mwaka na waraka mpya unataka shughuli hizo sasa kufanywa na wataalamu wa mipango miji kwa kushirikisha sekta mbalimbali kama vile sekta za maji, barabara, umeme nk.
Lukuvi alifanya maamuzi hayo leo tarehe 1 Juni 2021 katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Meru wakati akizingumza na madiwani wa halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya kusikiliza na kutatua kero za ardhi katika mkoa wa Arusha.
Alisema, kwa sasa waraka huo ameufuta mpaka utakapotolewa mwingine wenye maelekezo yatakayokuwa na tija na kusisitiza kuwa haiwezekani kuwaondoa madiwani kupitisha mipango ya uendelezaji miji katika halmashauri zake kwa kuwa mamlaka ya upangaji bado ziko chini halmashauri.
" Nimeamua kuufuta waraka namba moja unaokataza madiwani kupanga mipango ya uendelezaji miji katika halmashauri zenu, huwezi kuwa na halmashauri inayoshindwa kupitisha au kubariki mipango ya wilaya katika matumizi ya ardhi" alisema Lukuvi.
Post a Comment