HUSSEIN MWINYI AKUTANA NA PHILIP MPANGO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philp Esdori Mpango ambapo viongozi hao kwa pamoja walisisitiza haja ya kuendeleza mashirikiano yaliopo kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Viongozi hao walifanya mazungumzo hayo leo katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar ambapo mazungumzo hayo pia, yalihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
 
Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alimueleza Dk. Mpango kuwa anafarajika na juhudi kubwa zinazoendelea za mashirikiano yaliyopo ya Muungano ambapo kila siku zinapokwenda ushirikiano huo unazidi kuimarika.
 
Rais Dk.Mwinyi alieleza kuwa kutokana na mashirikiano hayo yaliopo yamepelekea changamoto zilizopo zinaweza kushughulikiwa kwa haraka  kwa azma ya kuweza kuijenga nchi katika pande zote mbili za Muungano.
 
Akieleza kuhusu suala zima la mazingira, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa licha ya kuwa masuala ya Mazingira si ya Muungano lakini jambo hilo lina umuhimu wa kushughulikiwa kwa pamoja kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Alieleza kuwa uharibifu wa mazingira si jambo la kubezwa  hasa katika visiwa vya Unguja na Pemba, hivyo kuna kila sababu ya kuimarisha ushirikiano katika jambo hilo.
 
Aliongeza kuwa pamekuwepo mashirikiano mazuri kati ya pande mbili hizo hata katika mambo yasiyohusiana na Muungano ambapo hata kwa upande  Wizara za Zanzibar zimeweza kupata fursa ya kujifunza mambo kadhaa kutoka katika upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo uzoefu ni mkubwa zaidi.

No comments