KESHA LA ASUBUHI
JUMATATU, MEI, 3, 2021
SOMO: MWALIKO WA MBINGUNI
Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.
Luka 14:11.
Hebu asiwepo mtu ajikwezaye, akijizungumzia mwenyewe, akisifia uwezo wake, akijionyesha maarifa yake, na akiendekeza majivuno. Hebu mtu asitafute kuchana kazi ya wengine ambao hawafanyi kazi kulingana na kipimo chake. Mwalimu wa mbinguni anatupatia mwaliko, "Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu.
Kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi." (Mathayo 11:28-30).
Kristo hakuwa anajitumainia nafsi, mwenye kushikilia itikadi, au mwenye majivuno. Alitangaza, “Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile.” (Yohana 5:19)
Hakuna mtu mwenye haki ya kudhani kwamba anajimiliki. Na hakuna mtu mwenye kitu chochote kizuri awezacho kukiita chake mwenyewe. Kila mwanadamu, kila kitu, ni mali ya Bwana. Yote mwanadamu anayoyapokea kutoka katika ukarimu wa mbinguni bado ni ya Bwana. Chochote kile tulichonacho ambacho ni cha thamani, tunapaswa kutumia kwa manufaa ya wanadamu wenzetu, ili waweze kuwa watendakazi wa thamani.
Kila nguvu, kila kipaji, ni talanta ambayo inapaswa kuchangia katika utukufu wa Mungu kwa kutumia katika huduma Yake. Uwezo wetu uliotolewa na Mungu haupaswi kufanywa ili kutumikia maslahi ya kibinafsi. Daima tunapaswa kuwa tayari kutoa, kuwaruhusu wengine wajue kila tunachokijua na tunapaswa kufurahi, ikiwa uwezo wetu utatumika utatengeneza nguvu na akili ya juu zaidi kuliko ile tuliyonayo.
Karama za Mungu hazipaswi kutumika kwa ajili ya kuitukuza nafsi, lakini zinapaswa kutumika, ili kwamba Ajipatie utukufu Wake. Hebu asiwepo ambaye anatafuta ukuu, furaha, au kujiinua kwa kukengeusha matumizi sahihi ya uwezo ambao amepewa; maana kwa kufanya hivyo anamwaibisha Mtoaji, na anashindwa kutimiza kusudi ambalo kwalo aliumbwa. Uwezo wetu wote unatoka kwa Mungu, na unapaswa kutumiwa kwa utukufu Wake...
Hakuna mtu mwenye sababu hata iliyo ndogo sana ya kujigamba. Hakuna mwenye sababu ya kujitukuza au kujiinua, hata pale ambapo anafanya vizuri sana.
0 Comments