KESHA LA ASUBUHI
JUMATANO, MEI, 26, 2021
SOMO: KUDAI FADHILA
Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.
Mathayo 7:13, 14.
Fanya chochote unachoweza na njia itafunguliwa mbele yako. Kila wakati ni wa thamani. Roho ambazo hazijampokea Kristo zinapaswa kuhimizwa zishikilie tumaini la injili .... Hatupaswi kuishi duniani hapa ili tujifurahishe sisi wenyewe. Tuna kazi kubwa sana ya kufanya kila siku ya maisha yetu. Tunatazama kwa imani mambo ambayo hayaonekani na kwa kufanya hivyo tunashindwa kuona majaribu na shida zilizopo njiani. Mbinguni ni nyumbani kwetu. Hatuthubutu kujihatarisha kupoteza lile tumaini ambalo tumekuwa nalo kwa muda mrefu, la kumwona Yesu kama Alivyo na kwa kufanywa kuwa kama Yeye. Tunaamini utalinda hatua zako. Ishi maisha ya maombi na imani kisha shinda taji ya utukufu isiyoisha.
Hakuna njia nyingine yoyote kwa ajili yetu kuokolewa isipokuwa njia ile ambayo imewekwa na Mkombozi wetu. Katika maisha yake hapa duniani, ametupatia kielelezo halisi cha kujikana nafsi na kujitoa sadaka jambo ambalo anatamani sisi tulifanye. Kristo anasema, “Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka.” (Yohana 6:38).
Hatuwezi kuwa Wakristo wakati tunaishi ili tujifurahishe wenyewe. Tunapaswa kuingia kupitia njia iliyonyooka ya kujikana nafsi, ikiwa tutamfuata Bwana wetu. Njia hii iliyonyooka ya kujikana nafsi ni nyembamba sana kwa wengi kutoweza kuiendea isipokuwa wale ambao wanaonesha utauwa. Wanataka njia rahisi na wanaendea njia nyinginezo. Wanakataa kuzifuata nyayo za Mkombozi wetu.
Kristo anawaita hao wote kuwa ni wezi na wanyang’anyi. Wanachukua jina la Mkristo, ambalo si la kwao, kwa sababu katika maisha yao hawamwakilishi Kristo. Wanadai upendeleo ambao ni wa wana wa Mungu wakati wao si Wake. Wanaishi maisha ya ubinafsi hapa duniani na hawajafanya kitu chochote kwa ajili ya kweli na wokovu wa roho kama ambavyo wangepaswa kufanya. Ni huzuni kweli kwa watu hawa waliojidanganya. Kamwe hawataiona mbingu, kwa sababu hawapo tayari kubeba aibu, fedheha ambayo Yesu aliibeba kwa ajili yako.
Wapendwa watoto, hebu Kristo akae mioyoni mwenu na mtawapenda wote ambao Kristo alikufa kwa ajili yao, na mtafanya yote mwezayo ili muwaokoe.
—Barua ya 30, Mei 26, 1874 kwa watoto wake.
0 Comments