KESHA LA ASUBUHI
JUMATATU, MEI, 24, 2021
SOMO: ARI YA KUUJUA UKWELI
Naye BWANA, yeye ndiye atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike.
Kumbukumbu la Torati 31:8.
Hakuna kitu chochote katika ulimwengu huu, si fursa au furaha za ulimwengu huu zinaweza kuchukua nafasi ya uwepo na upendeleo wa Mungu. Bila Yeye kama rafiki na sehemu yetu, kwa kweli tunakuwa peke yetu. Tunaweza kuwa na marafiki wengine wengi, lakini hawawezi kuwa kama Kristo alivyo kwetu.
Wale wanaotamani kupata msamaha wa makosa ya wakati uliopita wanapaswa kuja kwa Kristo kama walivyo, wakisema, “Bwana ingawa nimenunuliwa kwa gharama, na mimi ni mali Yako, huko nyuma nilikataa kujitoa Kwako. Sasa ninakiri kwamba mimi sijimiliki, kwamba siwezi kufanya kama nipendavyo. Nitwae jinsi nilivyo, masikini, kiumbe mwenye dhambi, na nioshe na kunitakasa dhidi ya dhambi zote kwa kuchukua dhambi yangu kuwa ya kwako. Sistahili hili, lakini ni wewe pekee ndiye unayeweza kuniokoa. Iondoe dhambi yangu na unipatie haki Yako. Sitaki kusalia dhambini kwa siku hata moja zaidi. Nipatie haki Yako, na uniondoe katika uasi wote wa sheria yako takatifu.”
Usimwekee mipaka Mtakatifu wa Israeli. Uwe na shauku ya kuona udhihirisho zaidi wa upendo Wake, ili uweze kuwavuta wengine wauone wema wake...
Bwana ameahidi ukamilifu wake wa utukufu kwamba wale ambao watamtafuta kwa unyenyekevu wa moyo, wakitubu dhambi zao, watamwona wa thamani katika roho zao. Lakini wale wanaokataa kutii, kwa hofu ya kuwapoteza marafiki wa duniani, hawawezi kuwa marafiki wa Mungu.
Tii, tii, kwa ajili ya Kristo na kwa ajili ya roho yako. Tii kile ambacho dhamiri yako inakuambia ni ukweli. Kubali neema na haki ya Kristo. Mungu anakuita kwa upole, “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu. Kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi” (Mathayo 11:28-30).
Ikiwa utakataa mwaliko wa kutubu, kuwa huru dhidi ya dhambi, siku kubwa ya Mungu itakukuta huna msaada, ukiwa huna kimbilio, usiyetii, mwasi wa sheria Yake. Kwa hiyo hataweza kukupatia nafasi katika ufalme Wake. Mungu akusaidie uje sasa, ndilo ombi langu.
—Barua ya 80, Mei 24, 1900,, kwa mshiriki wa kawaida nchini Australia.
0 Comments