Advertisement

Responsive Advertisement

KUTOKA MAKTABA NA DEO MWANASOKA

MOURINHO ATAFANYA CHOCHOTE KWA AJILI YA USHINDI.

Mourinho alimtuhumu kocha wa Barcelona, Frank Rijkaard kuwa alikwenda kwenye chumba cha waamuzi kuwashawishi wakati wa mapumziko, hatua ya 16 bora kati ya Barcelona na Chelsea 2005.

UEFA walipeleleza na kugundua Mourinho alidanganya, wakamfungia kuisimamia Chelsea katika michezo miwili ya robo fainali ya klabu bingwa Ulaya, Chelsea dhidi ya Bayern Munich.

Mourinho hakutakiwa kuwepo kwenye eneo la ufundi siku ya mchezo, hakutakiwa kuingia chumbani wala kuzungumza na wachezaji. Ila aliruhusiwa kutazama kutoka jukwaani.

Siku ya mchezo, Mourinho alifika uwanjani mapema sana kabla ya kila mtu. Kabla hata mashabiki hawajaanza kuingia. Akaelekea moja kwa moja chumbani kuisubiri Chelsea.

Chelsea ilipofika alizungumza, kisha akawaruhusu waende kupasha misuli kabla ya kuanza mchezo. Kumbuka hakutakiwa kuingia chumbani wala kukutana na wachezaji siku ya mchezo.

Tatizo lilikuja wakati wa kutoka, wasimamizi wa UEFA walikuwa macho kuhakikisha Mourinho haingii chumbani. Kama angeingia angepewa adhabu kali zaidi. Kumbe wakati wanamsubiri nje yeye tayari alikuwa ndani.

Mourinho tayari alikuwa na mbinu ya kutoka chumbani. Alimuita 'kit man' wa Chelsea, kisha akamuambia akamuelekeza apakue jezi zote kwenye kile kigari cha kubebea jezi.

Jezi zilipotolewa, Mourinho akaingia yeye kisha akamuelekeza ampeleke mpaka mlango wa nyuma wa jukwaa atakalokaa. Mourinho akaingia uwanjani na kukaa kila mtu akijua ametoka nyumbani.

Wakati wa mapumziko alirudia tena huu mchezo. Wachezaji wakiwa wanasubiri kocha msaidizi azungumze, wakashangaa kigari cha kubebea jezi kinaingia chumbani halafu jezi zinatolewa ndani yake anatokea Jose Mourinho na kuzungumza.

Chelsea walishinda 4-2. Huyu ndiyo Mourinho aliye tayari kufanya chochote kwa ajili ya ushindi.
.
✍Na @deo_mwanasoka

Post a Comment

0 Comments