ASKOFU NOVATUS BALOZI MPYA VATICAN


Askofu mkuu Novatus Rugambwa alizaliwa tarehe 8 Oktoba 1957, Katika Jimbo Katoliki la Bukoba. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre mikononi mwa Hayati Askofu Nestorius Timanywa kunako tarehe 6 Julai 1986.. Akajiunga na utume wa kidiplomasia mjini Vatican hapo tarehe 1 Julai 1991. Bahari ya Pacific ni eneo lake la "kujidai hadi raha".


Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.  – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Jumanne tarehe 30 Machi 2021 amemteuwa Askofu mkuu Novatus Rugambwa kuwa Balozi mpya wa Vatican kwenye Jamhuri ya Microsia, iliyoko Magharibi mwa Bahari ya Pacific. Wakati huo huo ataendelea kuwa ni Balozi wa Vatican kwenye Visiwa vya Marshall, Kiribati, Nauru na Tonga. Ataendelea pia kuwa ni Balozi wa Vatican nchini New Zealand, Fiji, Palau na Mwakilishi wa Kitume kwenye Bahari ya Pacific. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Novatus Rugambwa alizaliwa tarehe 8 Oktoba 1957, Katika Jimbo Katoliki la Bukoba nchini Tanzania. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre mikononi mwa Hayati Askofu Nestorius Timanywa kunako tarehe 6 Julai 1986. Akajiunga na utume wa kidiplomasia mjini Vatican hapo tarehe 1 Julai 1991.

Baada ya kufanya kazi mbali mbali katika Balozi za Vatican, kunako tarehe 28 Juni 2007 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa XVI akamteuwa kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum. Ilipofika tarehe 6 Februari, 2010, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, akamteuwa kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Angola, Sao Tome na Principe na kuwekwa wakfu kuwa Askofu mkuu na Kardinali Tarcisio Bertone, aliyekuwa Katibu mkuu wa Vatican kwa wakati ule hapo tarehe 18 Machi 2010. Na tarehe 5 Machi 2015 akateuliwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Honduras. Tarehe 29 Machi 2019, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Balozi wa Vatican huko New Zealand na mwakilishi wa kitume kwenye visiwa vya Bahari ya Pacific. Na ilipogota tarehe 30 Machi 2021, Baba Mtakatifu Francisko amemwongezea tena majukumu kwa kumteua kuwa ni Balozi mpya wa Vatican kwenye Jamhuri ya Microsia, iliyoko Magharibi mwa Bahari ya Pacific.

Askofu mkuu Novatus

No comments