majaliwa: rc njombe fuatilia madai ya wakulima wa chai
Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo ianzishe minada ya kuuza zao la chai katika ukanda wa maeneo yanayozalisha zao hilo ili kuwarahishia wakulima kupata soko la uhakika na kuacha kutegemea minada ya nje ya nchi.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Jumatano Machi 10, 2021 katika kikao na wadau wa zao la chai kilichofanyika katika ukumbi wa Johnson, mjini Njombe. Amesema Serikali itasimamia kikamilifu zao hilo na kuhakikisha wahusika wananufaika.
Amesema dhamira ya Serikali ni kuona zao hilo linapata mafanikio, hivyo amewataka watendaji wafuatilie kuhakikisha wakulima wote wananufaika na zao hilo. ”Lazima wakulima walipwe fedha zao kwa wakati ili waweze kuhudumia mashamba yao na kukidhi mahitaji yao.”
ADVERTISEMENT
Amesema zao la chai ni mojawapo ya mazao ya kimkakati hapa nchini na kwamba Serikali imedhamiria kuimarisha kilimo cha zao hilo ili liendelee kuwa na tija kwa wakulima, wenye viwanda na Taifa kwa ujumla.
“Zao la chai ni miongoni mwa mazao muhimu ya kibiashara yanayoliingizia Taifa fedha za kigeni. Zao hili huliingizia Taifa zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni 60 kwa mwaka. Tukiboresha mikakati yetu litatuongezea fedha nyingi zaidi.”
Waziri Mkuu amesema zao la chai limechangia kutatua tatizo la ajira nchini ambapo watu zaidi ya 50,000 wameajiriwa viwandani na mashambani. Pia limetoa takribani ajira 2,000,000 zisizo za moja kwa moja. “Idadi hii haitoshi kulingana na ardhi nzuri tuliyonayo.”
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji waje nchini kujenga viwanda vya kuchakata zao la chai kwa kuwa nchi ina mazingira mazuri ya uwekezaji na malighafi ya kutosha pamoja na nishati ya uhakika.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema suala la ucheleweshwaji wa malipo linalofanywa na baadhi ya wamiliki wa viwanda vya chai halikubaliki, amewataka wawekezaji wote wawalipe wakulima fedha zao kwa wakati.
Kuhusu kuwepo kwa minada ya chai nchini, Waziri wa Kilimo amesema ifikapo mwezi Mei mwaka huu wanatarajia kufungua mnada wa kuuza chai jijini Dar es Salaam hali itakayosaidia kupatikana kwa soko la uhakika.
Naye, Mwenyekiti wa vikao vya wadau wa chai, Spika wa Bunge Mstaafu Anne Makinda ameiomba Serikali kuiwezesha Bodi ya Chai Tanzania (TBT) na Taasisi ya Utafiti wa zao la Chai (TRIT) kwa kuipatia vitendea kazi na wataalamu ili waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Njombe alimweleza Waziri Mkuu changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima wa zao mkoani Njombe kuwa ni pamoja na baadhi ya viwanda vinavyonunua majani mabichi ya chai kushindwa kuwalipa wakulima fedha zao kwa wakati.
Post a Comment