Mawifi na mashemeji mtuache "WANANDOA"

*NDOA, KAYA NA FAMILIA.*

*SOMO: KUWAACHA WAZAZI NA KUWA MWILI MMOJA.*

Mafungu makuu:
Mwanzo 2:24
*“Kwa hiyo mwanamume atamwacha Baba yake na Mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja"*


*Sikia, binti, utazame, utege sikio lako, Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako.*
Zaburi 45 :10


Kati ya matatizo yanayochangia Ndoa nyingi kutokuwa na AMANI ni suala la Wanandoa kutowaacha wazazi wao. Ni kweli damu ni nzito kuliko maji, lakini Mungu anatoa agizo la wanandoa kuanzisha himaya yao. Magomvi tunayoyashuhudia kati ya – Mawifi, Mama mkwe, wakamwana, Mashemeji na Baadhi ya wanandoa, yanatokana na kutoelewa agizo hili. Agizo la kuwaacha wazazi lina maana kubwa, baadhi ni hizi:


1. Wanandoa wasianzie maisha kwenye kaya za wazazi wao, yaani wasiishi na Familia za wazazi wao. Wanapaswa kuanzisha himaya yao, yenye uhuru kamili wa maamuzi juu ya maisha yao. Hivyo kuwa makini sana juu ya jambo hili.


2. Ndugu wasaidiwe, lakini wasipewe nafasi ya kiutawala, kuna mashemeji wanatoa Amri utafikiri ni nyumbani kwao. Mke ameolewa na mmoja, athaminiwe, mara nyingi akina Dada (Mawifi), wanaona wivu kwa kila kitu anachofanyiwa wifi yao, wanaume wanatakiwa kuwa na Msimamo juu ya wake zao, Mke ni Ubavu na ni mwili mmoja.


3. Siri za Mke na Mume zisitoke kwenda kwa Ndugu, labda kwa makubaliano inapobidi. Kuna wanandoa hawatulii, kila jambo lazima liende kwa Ndugu. Mara nyingi Dharau zinaanza kwa kutotunza Siri. Ukushindwa kuwa na hekima katika hili hakuna mafanikio katika Ndoa hiyo.



4. Inapolazimu kukaa na Wazee- mfano. Mama Mkwe, ni wajibu wa mwanamume kumlinda mke wake, mara nyingi akina Mama wakiwa kwa watoto wao wa kiume wanajitwalia Madaraka, na kujiona ni wa muhimu kuliko wakwe zao, atataka apatiwe mahitaji zaidi au sawa na mkwe wake. Wengine wanataka kufanana hadi nguo rangi za nguo. Wewe mwanamume tambua wajibu wako katika hili.


5. Kama mtakaa na Ndugu wa upande wowote, hakikisheni hawaingilii uhuru wenu wa Ndoa kwa namna yoyote ile.

6. Endapo kumetokea kutoelewana kati ya wanandoa, usipeleke mashitaka kwa wazazi wako, peleka mashitaka kwa wazazi wa mwenzio. Wazazi wako mara nyingi hawataona kosa lako, hivyo ni rahisi tatizo kutopata ufumbuzi.


Mawifi, Mashemeji, Akina Mama na Baba Mkwe, na wakamwana – Tafadharini sana waachieni wanandoa nafasi na Uhuru, hao ni mwili mmoja. Wanandoa msiogope mawimbi yakiwapata, Mungu yupo atawashindia Daima, anao uwezo wa kutuliza kila aina ya DHORUBA.
Kamwe msimwache  Mungu.

*MUNGU ATUSAIDIE TUNAPO YAZINGATIA HAYA.*
🙏🙏🙏

No comments