MGOGORO KKKT MAASKOFU WAMTUHUMU ASKOFU DK. SHOO

UKIMYA wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo umetajwa kuchochea kadhia ya migogoro inayolikumba kanisa hilo kwa sasa.RAI linaripoti.
Hoja ya uchochezi dhidi ya Askofu Dk. Shoo umepewa sura mbili, moja ni huenda anafurahishwa na hali inayoendelea kwa sasa ndani ya Kanisa au labda lipo kundi la watu kwenye mgogoro huo analiogopa.
Hayo yanaibuka wakati ambao Kanisa hilo linapitia wakati mgumu wa migogoro isiyokwisha kwenye baadhi ya kanda zake, hali inayotishia usalama wa baadhi ya maaskofu wake.
Miongoni mwa kanda zenye migogoro ni Kusini unayoihusisha sharika za Sumbawanga, Mtwara, Mafinga, Makete na Mpanda.
Maaskofu wa ukanda huo ndio wameibuka na kutoa shutuma hizo dhidi ya Askofu Dk. Shoo kwa madai kuwa wamechoshwa na ukimya wa kiongozi wao mkuu.
Kwa umoja wao maakofu hao wametoa tamko linalomtaka Askofu Dk. Shoo kuingilia kati migogoro hiyo haraka.
Maaskofu hao wameweka wazi kuwa ukimya wake katika jambo hilo hauna faida yoyote kwa Kanisa na kwamba ni vema akatoa tamko zito litakalochochea kupatikana kwa muafaka katika sharika hizo.
Ikumbukwe kuwa katika siku za hivi karibuni kanisa hilo limekuwa katika dimbwi la migogoro iliyofikia hatua ya Askofu wa Dayosisi ya Ziwa Tanganyika, Ambele Mwaipopo kupigwa jiwe kichwani na waumini wake.
Askofu Mwaipopo alikutana na dhahama hilo Mei 6, mwaka huu wakati akiendesha ibada kwenye usharika wa Sumbawanga mjini.
Kutokana na kadhia hiyo baadhi ya maaskofu na waumini wamesema licha ya Kanisa hilo kuwa na umri wa zaidi ya miaka 50 sasa tangu kuunganika kwa makanisa saba ya Kilutheri nchini, tukio hilo ni la aina yake tangu kuasisiwa kwake mwaka 1963.
KAULI ZA MAASKOFU
Akizungumzia mkasa huo Askofu Mwaipopo alisema askofu mkuu anatakiwa kuvunja ukimya na kukabiliana na migogoro mbalimbali inayolikabili kanisa hilo.
“Kwa sababu kushindwa kuwachukulia hatua watu wanaotajwa kuhusika na matukio ya uvunjifu wa amani na wale wanaotoka nje ya misingi ya kanisa ni kitendo kinachotia doa kanisa,” alisema.
Aidha, alisema wakati kanisa linaandaa waraka uliosomwa Aprili mwaka huu kwenye sharika mbalimbali nchini, kuna mambo muhimu mbayo yalijadiliwa na yalipaswa kufanyiwa kazi na ofisi kuu hasa masuala ya migogoro yanayoendelea katika sharika za ukanda wa kusini.
Alisema chanzo cha migogoro hiyo inaonekana kufanana na ndio sababu ya dayosisi za Kusini kulifikisha suala hilo kwenye ofisi mama ili yafanyiwe utatuzi, lakini cha kushangaza licha ya kuwasilisha taarifa hizo bado mkuu huyo wa kanisa ameonekana kuwa mgumu kuyafanyia kazi jambo linalowatia hofu na shaka kwamba huenda anafurahjia au kuna kundi analiogopa.
Alisema sasa maaskofu hawana uhuru kutokana na ubabe unaoendeshwa na Mkuu huyo wa kanisa hasa kwenye usalama wao jambo ambalo halikubaliki.
“Mwaka huu kuna mmoja wa wachungaji kutoka Kaskazini alipigwa na watu wasiojulikana, Halmashauri Kuu ya Kanisa iliketi ikiongozwa na mwenyekiti ambaye ni mkuu wa kanisa, mambo mengi yalijadiliwa lakini suala hili la migogoro lilimpa kigugumizi licha ya matamko mengi kutolewa,” alisema.
Alisema, Halmashauri ya KKKT dayosisi ya Ziwa Tanganyika inasikitika sana kwa kitendo cha Mkuu huyo kunyamaza kimya na ndio sababu imeamua kuweka bayana kwamba Mkuu wa Kanisa hilo Dk. Fredrick Shoo anahusika na migogoro hiyo kwani, ukimya wa kiongozi huyo kwenye suala nyeti la askofu kupigwa mawe ni kipimo tosha.
“Iweje Mkuu wa KKKT kukaa kimya katika tukio hili hatarishi na nyeti sana? Mbona anaonekana kukemea mengi hili kwanini limemponyoka? Halmashauri kuu ya KKKT Ziwa Tanganyika ni lazima tumhusishe na mgogoro huu kwa sababu watendao uovu ni vijana wake, tunamuomba na kumsihi kama msemaji wa kanisa atoe neno la karipio na awakemee vijana wake hawa na wote wanaojihusisha na migogoro,” alisema.
Aidha, Askofu wa Dayosisi ya Kusini, Isaya Mengele ambaye pia ni Mwenyekiti wa Maaskofu Ukanda wa Kusini alisema ili kupatikana kwa mchakato wa amani kipindi cha mpito kinahitajika ili kuokoa nyoyo za watu ambao wamekengeuka.
Alisema, kunapaswa kuwekwa mchakato endelevu wa kutafuta amani, na kwamba si vema wakae mbali bila kusema na kufanya jambo, na kwamba tukio linaloendelea Sumbawanga linaweza kuifanya serikali inaweza kushindwa kutambua jitihada zinazofanyika kwa wahusika kushindwa kutamka neno.
Alisema, wote waliobahatika kulelewa kwa mapokeo ya amani ni tarajio ambalo serikali ilipaswa kuliona hivyo, lakini isiwe tatizo hivyo wameona wainuke washirikiane kusema na kuonekana mbele yao na kutoa shukrani zao hata kama msemaji mkuu ameamua kunyamaza.
“Si kwamba tulipaswa kuchelewa, lakini tulikuwa tunahoji je, kwa hali ilivyo sasa tutakuwa salama, na hili ndilo lililochangia wengi kusita kufika kutoa pole kwa mwenzetu na ndio sababu tumekuja wachache ili kuona hali halisi na wengine wafuate, sisi ni miongoni mwa maaskofu 13 ambao tumeamua kujitoa sadaka,”alisema.
Alisema, ni ujasiri wa ajabu kwa msharika kuthubutu kumrushia jiwe askofu ni sawa na kurushia jiwe Rais, lakini mambo yamekaa kimya na hali hiyo imewaletea doa kwenye kanisa na kuonekana kama ni tukio la kawaida kwani hakuna jambo linalo fanyika.
Alisema, doa hilo haligusi familia ya kanisa pekee, bali pia linagusa uwajibikaji wa vyombo vyetu kwa watu wake kwamba je, vinapeleka usalama kote wakati inatambulika kwamba changamoto ya usalama ipo mikononi mwa kanisa.
Aidha, alisema kanisa halina siasa wala chama kama ilivyo serikali ambayo haina dini, hivyo kanisa litabaki kuwa kitovu cha kuhubiri amani, umoja na upendo na si siasa kama viongozi wengine wanavyotarajia iwe.
Alisema, kwa sababu kanisa linaunganisha watu wote wenye itikadi mbalimbali za kidini na kisiasa hivyo likikumbatia sehemu moja basi ni lazima ligawanyike na nchi haitatawalika kwani dini na serikali vinategemeana.
“Nguvu yetu, usalama wetu ni kuwakusanya watu na si kuwagawa, tunaamini kuwakusanya watu kwa imani zao walie, wacheze na kucheka pamoja ila wakitoka nje ya kanisa waendelee na shughuli zao ambazo sisi hatupaswi kuziingilia kwani mbali na vitabu vya dini kuandika maandiko mbalimbali, lakini vitabu vya elimu navyo vimeeleza mambo ya ngoswe mwachie ngoswe hivyo hatupaswi kuyaingilia,”anasema.
Alisema, kazi ya kanisa ni kuwahimiza waumini wafanye shughuli zao kwa amani na utulivu, sasa inapotokea yameanza kuvurugika kwa watu wa imani na nia moja hapo tunaanza kupata maswali makubwa sana.
“Na ikifikia hapo ni lazima wajitafakari kwani ni changamoto kubwa na lazima wajihoji kwamba ni wapi wamekosea kati ya viongozi na watumishi ambao tumewapa wajibu wa kusimamia amani.
“Hakukuwa na sababu ya kanisa kuendelea kukumbatia migogoro ya kiimani inayoendelea kuibuka pasipo kuitafutia ufumbuzi halafu kanisa ndio linaonekana kuwa kinara kwa kuyasema ya watu wengine, huwezi kutoa kibanzi kwenye jicho la mwenzio wakati la kwako bado hujalichunguza.”
Askofu wa Dayosisi ya Kusini Magharibi Matamba, Job Mbwilo, alisema wakati umefika wa makanisa kurejea misingi ya kiimani na kuachana na imani za mihemuko ambazo zaidi zinaweza kuliteketeza kanisa.
Alisema, wakati umefika kwa makanisa kuanza kurekebisha baadhi ya vipengele kwani watu kabla hawajapewa mamlaka za kikanisa wanapaswa kuchunguzwa ili kufahamu tabia na mienendo yao ili kupunguza mipasuko isiyo kuwa na ulazima.
“Kabla ya mtu kupewa madaraka anapaswa kuhojiwa imani yake pamoja na itikadi zake kama vile itikadi ya siasa na utumishi wake kwani viashiria vingi vya migogoro vinaanzia huku,”alisema.
Alisema, mgogoro huu wa Sumbawanga ukiufuatili kwa haraka unabaini kuna mambo mengi yamejificha na zaidi ni siasa tu na tamaa binafsi hivyo wakati umefika kwa kanisa kuanza kuwachunguza watu wanaopewa dhamana ya kuliongoza kanisa kabla.
Mchungaji Sanga Mbilinyi, alisema wachungaji wanatakiwa kuzingatia viapo wanavyoviapa ili kuepuka migogoro ambayo wakati mwingine inaweza kuligawa kanisa.
“Mchungaji anapokula kiapo moja ya mambo ambayo hutamka ni kwamba, atalitumikia kanisa na watu wake ikiwa ni pamoja na kutii mamalaka za juu yake na kwamba yupo tayari kulitumikia kanisa mahala popote, hivyo hakuna sababu ya mchungaji kugoma kuondoka na jambo hilo linapotokea ni lazima watu wajitafakari,”anasema.
WAUMINI NAO WASEMA
Wakizungumzia hilo, baadhi ya waumini wa kanisa la KKKT, wameuomba uongozi wa juu kuhakikisha wanatatua matatizo yanayoendelea kwenye baadhi ya sharika zilizoainishwa ili kuondoa doa linaloweza kulichafua kanisa.
“Tumechoka na migogoro hii, inatia aibu kanisa, hadi inafika mahala tunaona bora tuhame dhehebu kutokana na migogoro isiyokuwa na tija na ukifuatilia zaidi ndani yake unakuta kuna maslahi ya kifedha, kikabila na kisiasa sisi tumechoka,”alisema Janet Peter.
Ibrahamu Jakobo, Hosea Charles na Elizabeth Mathayo kwa pamoja wanasema kama mambo hayo yataachwa basi ukabila unaweza kuligawa kanisa hilo.
Walisema hakukuwa na sababu ya kiongozi wa juu kusambaza barua kwenye dayosisi mbalimba zinazowataka wachungaji wanaotoka kaskazini kurejea kwao Kilimanjaro tendo hilo ni la kibaguzi na linapaswa kukemewa.
“Viapo vya utii vinawekwa pembeni, kiongozi mkubwa huwezi kutamka maneno hayo eti vijana wangu warejee nyumbani kisa ni wachaga, hili hatukubaliani nalo na kama litaachwa basi dhana hii ya ubaguzi inaweza kusababisha vita,”anasema.
Hata hivyo, akizungumzia mgogoro wa kikanisa uliokuwa unaendelea katika Sharika ya Sumbawanga Mjini, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk. Halphan Haule, amewataka viongozi wa kanisa hilo kuhakikisha wanatekeleza shughuli zao kwa kufuata utaratibu na kuzingatia misingi ya kanisa na kuheshemu katiba yao.
“Makanisa yanapoanzishwa husajiliwa na serikali na Katiba huwasilishwa hivyo kama kuna mambo yatafanyika kinyume cha katiba hiyo basi serikali haitasita kuwachukulia hatua ikiwa ni pamoja na kuyafuta makanisa ambayo yatakuwa vinara vya uchochezi,”aliasema.
ASKOFU DK. SHOO KIMYA
RAI lilifanya jitihada za kumtafuta Askofu Dk. Shoo kwa zaidi ya wiki moja bila mafanikio, hata utaratibu wa kuongea nae kwa simu ulipofanyika nao haukuzaa matunda na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakukuwa na mrejesho.
ORODHA YA VIONGOZI KKKT
Mwaka 1963 KKKT lilianzishwa likiwa chini ya baba Askofu Stephano Moshi hadi mwaka 1976 na kufuatia Dk. Sebastian Kolowa kuanzia mwaka 1976 hadi mwaka 1992.
Aidha kuanzia mwaka 1992 hadi mwaka 2007 liliongozwa na Dk. Samsoni Mshemba ambaye naye alimuachia Dk. Alex Malasusa hadi mwaka 2015 ambaye amemwachia Dk. Shoo.
source:-Raia.co.tz
Post a Comment