WIZARA YA AFYA YAPOKEA MAONI KUTOKA KWA WADAU MBALIMBALI KUHUSU UENDESHAJI WA MTIHANI WA AWALI (Pre-Intership Examination) KWA MADAKTARI WATARAJIWA
Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imepokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu uendeshaji wa mtihani wa awali (pre-internship examination) kwa Madaktari watarajali walio katika fani ya Udaktari, Udaktari wa meno na utaalamu wa Afya shirikishi kwa mujibu wa Sheria ya Madaktari, Madaktari wa Meno na Wataalamu wa Afya Shirikishi, Sura ya 152 pamoja na Kanuni ya Mafunzo ya Utarajali, Tangazo la Serikali Na. 703 la mwaka 2018.
Hivyo, Waziri wa Afya, Mhe Ummy Ally Mwalimu (Mb), baada ya kushauriana na watalaamu kuhusu utekelezaji bora wa Kanuni za mafunzo hayo, ameamua kufanya yafuatayo:
1. Mtihani wa awali (pre-internship examination) kwa Madaktari Watarajali uendelee kufanyika bila kumzuia mtarajali kujiunga na mafunzo ya utarajali.
2. Matokeo ya mtihani huo yatakuwa sehemu ya matokeo ya mtihani wa mwisho (post-internship examination) unaofanyika mara baada ya mhitimu kumaliza mafunzo yake ya utarajali.
3. Watarajaliwa wote waliofanya mtihani huo wa awali na kushindwa kuendelea na mafunzo ya utarajali, Baraza linaelekezwa kuwapa usajili wa muda na kuweka utaratibu utakaowezesha kuendelea na mafunzo ya utarajali katika Hospitali mbalimbali.
Wizara imesema inatambua umuhimu wa mtihani wa awali katika kulinda taaluma ya udaktari na utakuwa chachu ya Madaktari Watarajali kuzingatia mafunzo yao na kuwaandaa kufanya vyema kwenye mtihani wa baada ya mafunzo kwa vitendo (post-internship examination) ambao utaendelea kama kawaida.
Aidha, mtihani wa awali utaendelea kutoa picha ya viwango vya ufundishaji katika vyuo vya udaktari na kuendelea kuviboresha kupitia tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU).
Vilevile, Wizara imepokea maoni ya Wanataaluma kuhusu Mafunzo endelevu ya kitaaluma (Continuing Professional Development) kwa ajili ya kuhuisha leseni, hivyo Baraza lifanye tathmini ya gharama na utaratibu unaofanyika sasa mapema iwezekanavyo wakati utekelezaji ukiendelea. Mafunzo haya yanalinda ubora na uendelevu wa taaluma ya udaktari.
Wizara imesema itaendelea kupokea maoni na ushauri ili kuendelea kuboresha mafunzo na viwango vya taaluma ya udaktari nchini.
Utekelezaji wa tamko hili umeanza mara moja.
Post a Comment