WAJUMBE CCM WAMPONGEZA RAIS SAMIA LEO

Kikao cha kawaida cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kimefanyika Jumanne Juni 29, 2021 chini ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ndugu Samia Suluhu Hassan katika ukumbi wa White House Dodoma.

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa wameazimia na kutoa tamko la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Husein Ali Mwinyi kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuiongoza nchi na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM 2020 - 2025.

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa wamebainisha kuwa tokea nchi ilipopata msiba mkubwa wa kuondokewa na aliyekuwa Rais, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, ndani ya siku mia moja za uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa na kuonyesha dira ya serikali anayoiongoza kuwa inazingatia uadilifu, Utawala wa Sheria, Haki, Usawa, kuimarisha misingi ya demokrasia, umoja na mshikamano zaidi kuendelea kutunza Amani na usalama wa nchi.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesisitiza juu ya azma ya Serikali inayoiyongoza kuhakikisha inakamilisha na kuiratibu vyema miradi yote ya kimkakati iliyoanzishwa na inayoendelea kutekelezwa sambamba na kuhakisha uchumi wa nchi unakuwa kwa kasi.

“Miradi yote iliyopo kwenye maeneo yenu viongozi wa CCM mnao wajibu wa kuifatilia, kuikagua na kujua uendelevu wake bila uwoga kwani huo ni wajibu wenu wa msingi katika kutusimamia Serikali, hilo liende sambamba na kuhakikisha mnasaidia kuona mapato ya Serikali hayapotei katika vyanzo vyote vya ukusanyaji, ikumbukwe ninyi ndio kioo cha kutumurika, kwavile ilani inayotekelezwa ni ya Chama Cha Mapinduzi lazima ifanikiwe kwa kiwango kikubwa” Ndugu Samia Suluhu Hasasan Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

No comments