SERIKALI YASEMA JEMBE LA MKONO LIENDE MAKUMBUSHO
Wadau wa zana za kilimo wamekutana leo tarehe 30/6/2021 katika ukumbi wa Royal Village jijini Dodoma kwa lengo la kujadili namna bora ya kuongeza matumizi ya zana za kilimo katika mnyororo wa uzalishaji na tija kwenye mikoa ya Singida, Manyara, Arusha, Mbeya,Iringa,Dodoma ,Simiyu na Njombe.
Bw. Philbert Lutare Mkurugenzi wa Rasilimali watu Wizara ya Kilimo kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu amesema kuwa kumekuwa na mabadiliko makubwa hasa katika eneo la ukatuaji kwa kutumia zana za kisasa za kilimo hususani matrekta. Katika mwaka 2020, jumla ya matrekta makubwa 1,124 na matrekta madogo ya mkono 459 yameingizwa nchini ambapo imesababisha matumizi ya matrekta kuongezeka hadi kufikia asilimia 23 kutoka asilimia 20 mwaka 2018.
Hata hivyo Lutare ameendelea kusema kuwa katika kipindi hicho matumizi ya wanyamakazi na jembe la mkono yamefikia asilimia 27 na asilimia 50 mtawalia ukilinganisha 27 kwa wanyamakazi na 53 kwa zana za mkono.
Aidha, Lutare amesema kuwa matumizi ya zana za kilimo kama vinu vya kutwangia na mawe ya kusagia umepungua na tathmini imeonyesha nchini kuna mashine za kusaga mahindi zaidi ya 25,000, mashine za kusindika mpunga 4,647 na mashine za kukamua mafuta 1,905.
“ili kuweza kumsaidia Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kukuza uchumi wa nchi ni vyema jembe la mkono tulipeleke makumbusho ili vizazi vijavyo vijifunze kuwa kulikuwa na jembe la mkono,tutoke hapa tulipo.”alisema Lutare
Naye Meneja Mkuu wa Chama cha wakulima Bw.Stephen Henry Marealle amesema kuwa ameridhishwa na kauli hiyo ya kuacha jembe la mkono kwani imeleta faraja kwa mkulima baada ya kujiuliza kwa muda mrefu ni lini jembe hilo wataachana nalo.
Aidha, Stephen amemuomba Lutare kuwa kwa kipindi hiki trekta zitakazoingizwa nchini ziwe na ubora kwani kwa kipindi kilichopita hakuna mkulima aliyefaidika na matrekta hayo. Pia ameomba kushuka kwa bei ya mbegu za mazao mfano aithan inauzwa 35,000 na wangependa ishuke hadi 7000 hadi 8000.
Wadau waliohudhuria mkutano huo ni wauzaji wa zana za kilimo,watumiaji,watoa huduma ya ukodishaji wa zana za kilimo kwa mkulima.
Post a Comment