RAIS SAMIA AMEDHAMILIA KULETA MAENDELEO-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wananchi kuiunga mkono Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuwa ina nia thabiti ya kuwaletea maendeleo.

Ametoa kauli hiyo (Jumatatu Juni 7,2021) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa kata za Nandagala, Likunja, Nambilanje na Ruangwa Mjini mkoa wa Lindi.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia imetoa Shilingi bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa
Sekondari katika kata ya Likunja ambayo itakuwa ni kubwa kuliko zote wilayani Ruangwa.

Aliongeza kuwa Shule hiyo itakuwa na madarasa 13, matundu ya vyoo 30. jengo la utawala maabara 2 kubwa,
mabweni 4, nyumba za walimu 2, bwalo na jiko "pia vita jengwa viwanja vya michezo katika shule hiyo".

Amesema Wilaya ya Ruangwa imedhamiria kuhakikisha inajenga shule za sekondari katika kata ambazo hazina shule hizo lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba watoto wote wanapata fursa ya kusoma. 

Kuhusu huduma ya maji safi na salama, Waziri Mkuu amesema Wizara ya Maji kupitia Wakala wa Maji Safi na
Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) imeanza kufanya usanifu wa mradi wa maji kutoka eneo la Ndanda ambako kuna chanzo kikubwa cha maji cha Mbwinji ili kuyafikisha Ruangwa.

Amesema kuwa mradi huo utavinufaisha vijiji vya Mbecha, Michenga, Chimbira A na B. Nandagala, Namahema, Mpumbe, Nkowe, Mitoke na Likunja.

Akizungumzia sekta ya umeme, Waziri Mkuu amesema kazi ya usambazaji umeme vijijini na maeneo yaliyopo nje ya miji inaendelea vizuri na wale wote ambao wamelipia gharama za kuunganishiwa umeme wataunganishwa kupitia mpango wa REA.

No comments