JAFO AZITAKA KUMBI ZA STAREHE SAUTI ZISIZIDI VIWANGO

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo amewaagiza wamiliki wa kumbi za starehe na burudani kuhakikisha sauti zitokanazo na shughuli zao hazizidi viwango vinavyokubalika kwa mujibu wa sheria.

Waziri Jafo amesema hayo Jana Jijini Dodoma wakati wa kutoa Tamko kwa umma juu ya udhibiti wa uchafuzi wa mazingira utokanao na kelele na mitetemo na kuwaagiza wamiliki wa maeneo ya burudani na starehe kuzingatia matumizi ya vipima kelele na vizuia sauti kama ilivyoelekezwa kwenye masharti yote ya leseni zao.

“Katika kuhakikisha tunalinda Afya ya Jamii kutokana na athari zitokanazo na kelele na mitetemo Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI; Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji; Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto; Wizara ya Viwanda na Biashara; Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi; Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi; na Wizara ya Habari, Sanaa na Michezo tunaelekeza Kila Mwananchi ahakikishe shughuli anazofanya hazisababishi kero ya kelele na mitetemo” Jafo alisisitiza.

Aidha, Waziri huyo amesema kasi ya ukuaji wa uchumi inaenda sambamba na ongezeko la shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii ambazo zinaambatana na ongezeko la uchafuzi wa mazingira unaotokana na Kelele na Mitetemo na kusababisha athari za kiafya na kimazingira kwa jamii.

Aliongeza kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa ya maendeleo katika Nyanja za kiuchumi na kijamii kutokana na Mipango madhubuti ya Serikali kwenye Uwekezaji katika Sekta mbalimbali.

Hivyo, ameutaka umma wa Watanzania kuhakikisha agenda ya kelele na mitetemo inakuwepo kwenye mikutano ya wakazi na kuwaomba wananchi kutoa taarifa kuhusu kero na mitetemo kwa Ofisi za Serikali za Mitaa au NEMC kwa Namba za bure (0800110115 au 0800110117 au 0800110116)

Amesema yeyote atakayesababisha kero zitokanazo na kelele na mitetemo kinyume na Kanuni za Usimamizi wa Mazingira (Udhibiti wa kelele na mitetemo) za mwaka 2015 atakuwa amevunja sheria na adhabu yake ni faini isiyopungua shilingi milioni moja au kifungo kisichozidi miezi sita, sambamba na kufungiwa kwa biashara husika.

No comments