Advertisement

Responsive Advertisement

WATANZANIA WATAKIWA KUTOA USHIRIKIANO WAKATI WA SENSA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Jana Mei 22, 2021 amezindua kitabu cha mkakati wa usimamizi na utekelezaji wa Sensa ya watu na makazi ya Mwaka 2022, katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu Jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa watanzania kutoa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha utekelezaji wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika Agosti 28, 2022.
 
Amesema takwimu zitakazopatikana katika zoezi hilo zitatumiwa na Serikali katika utungaji, ufuatiliaji na uboreshaji wa sera mbalimbali pamoja na kufanya maamuzi kwa kuzingatia vigezo vya kitakwimu. 
 
“Ni dhahiri kuwa, takwimu rasmi zitaiwezesha Serikali ya Awamu ya Sita na wadau wengine kufuatilia na kutathmini Malengo yaliyofikiwa katika kutekeleza Mipango ya Maendeleo iliyokusudiwa kwa lengo la kukuza uchumi na kupunguza umaskini na hatimae kufikia Dira yenyewe”.
 
Aidha, Waziri Mkuu amesema takwimu rasmi zitaiwezesha Serikali kukabiliana na changamoto mbalimbali zitakazojitokeza katika sekta zote za kiuchumi kwa kuwa zitatoa viashiria vya Uwajibikaji ndani ya Serikali.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla amesema kuwa hana shaka  na utendaji kazi wa ofisi za takwimu za Zanzibar na Tanzania Bara kwani ushirikiano wao ulifanya sensa ya mwaka 2012 kuwa bora barani Afrika na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha zoezi hili linafanyika kwa mafanikio

Post a Comment

0 Comments