RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza umuhimu wa kuwasaidia walimu wa madrasa na kuwachangia kwa hiari bila ya kusubiri kuombwa au kushurutishwa.
Alhaj Dk. Mwinyi ameyasema hayo janahuko katika uwanja wa Amaan Jijini Zanzibar katika hafla ya mashindano ya kuhifadhi Kur-an Kitaifa yaliyoandaliwa na Taasisi ya Maahil Irfaan kutoka Dar-es-Salaam na Taasisi ya kuhifadhisha Kurani Zanzibar kwa kushirikiana na Ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibar.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa dini na Serikali kutoka Zanzibar na Tanzania Bara akiwemo Rais Mstaafu wa Awamu ya Saba Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih, Mawaziri pamoja na wananchi mbali mbali.
Katika hotuba yake, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa ni vyema Wazazi wakaona kazi kubwa na ngumu inayofanywa na walimu wa madrasa ya kuwasomesha na kuwalea watoto na wawe tayari kuchangia kwa hiari bila kusubiri kushurutishwa.
Alisema kuwa katika mfumo wa maisha ya zamani ambao bado unaendelea katika sehemu zote za Unguja na Pemba walimu wa madrsa walijitewezesha wenyewe lakini katika uhalisia wa maisha ya sasa jambo hilo ni gumu hasa ikizingatiwa idadi ya wanafunzi katika madrsa imeongezeka.
Aliongeza kuwa walimu wanahitaji muda zaidi wa kuwasomesha na kuwasimamia wanafunzi wakati wa kudurusu hivyo ni vyema wema na ihsani hiyo ya kujenga utamaduni wa kupenda kuchangia madrasa ukathaminiwa.
0 Comments