RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kwamba kazi ni ibada hivyo amewataka wale wote walioajiriwa kufanya kazi watekeleze jukumu hilo ipasavyo na iwapo watafanya kinyume yake watakuwa wanafanya dhulma.
Alhaj Dk. Mwinyi ameyasema hayo jana alipokuwa akitoa salamu zake kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na wananchi wote mara baada ya Sala ya Ijumaa huko katika Masjid Aljalil, Mbuzini, Wilaya ya Magharibi “A”, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Katika salamu hizo Alhaj Dk. Mwinyi aliwataka wale wote walioajiriwa kufanya kazi watekeleze majukumu hayo ipasavyo na watakapofanya kinyume yake watakuwa wanadhulumu kwani watakuwa wakilipwa mishahara ambayo hawaitendei haki.
Alieleza kuwa wapo baadhi ya wamafanyakazi katika sekta ya umma hawatekelezi majumuku yao uipasavyo hivyo, alisisitiza kwamba ni vyema wakafanya kazi kama taratibu zilivyoelekeza ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa muda waliopangiwa.
Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kwamba maendeleo hayawezi kupatikana iwapo kutakuwa na dhulma ambayo haionekani kwani Serikali imeweka wafanyakazi ili kupata maendeleo.
Alisisitiza kwamba kila mmoja ajione ana wajibu mbele ya Mola wake wa kufanya kazi kwani kazi ni sehemu ya ibada katika kutekeleza jukumu hilo.
0 Comments