Hisia kali zimetawala katika mioyo ya mashabiki wa Simba na Yanga.. Presha inapanda, presha inashuka...
Mashabiki wa Simba wamepatwa na taharuki kusikia mkataba wa beki wa kushoto, Mohammed Hussein 'Tshabalala' umebakisha miezi miwili tu..
Presha inapanda zaidi wakisikia mazungumzo ya mkataba mpya yamesimama. Ni kama ilivyo kwa Kapombe, naye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu..
Siyo hao tu, wachezaji wengine watano pia wanamaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu huu.
Kwa upande wa Yanga, mashabiki wao wamekuwa na presha pia. Wanajiuliza kama Tshabalala na Kapombe watasaini kwao kweli. Nani asiyetaka Tshabalala na Kapombe wacheze katika timu yao? Hakuna.
Hawa ndio mabeki hodari zaidi wa pembeni nchini. Roho ya Simba na Taifa Stars.. Hawana mpinzani. Kwanini usiwatamani?
Hata hivyo kwa uzoefu wangu, sidhani kama Tshabalala na Kapombe wataenda Yanga. Sidhani.
Kinachofanyika sasa ni kutumia fursa vizuri. Ni kama vile ilivyokuwa kwa Chama. Ukishafahamu thamani yako, mkataba wako ukiwa unamalizika wala huna haja ya kuwa na papara.
Kama upo Simba, unakubali mazungumzo ya Yanga. Unawatamanisha kama unakwenda kwao. Kadri ofa ya Yanga inavyokuwa kubwa, ndivyo thamani yako inaongezeka pale ulipo.
Hii aliifanya Haruna Niyonzima miaka mingi sana pale Yanga. Kila mkataba wake ulipokaribia kumalizika, alihusishwa kwenda Simba, lakini hakwenda. Aliipandisha thamani yake pale Yanga kwa kutumia ofa za Simba. Ilipofika hatua Yanga ikawa haijiwezi ndio akaenda Simba kweli.
Wachezaji wengi wa Simba na Yanga wamekuwa wakitumia fursa hii vizuri. Mikataba yao ikielekea ukingoni lazima wajihusishe na kwenda timu pinzani. Wanajua faida yake.
Kuna kiungo mmoja wa Simba anajua kuitumia fursa hii vyema sana. Kila mkataba wake ukikaribia kumalizika huwa anazungumza na Yanga. Anawaaminisha kuwa anaenda kwao, lakini baadaye anapeleka mkataba huo Simba na kupata ulaji. Yaani Simba inampa mkataba kwa hofu kuwa huenda akaeda upande wa pili.
Kwa uzoefu wangu wa masuala ya usajili, sidhani kama Tshabalala na Kapombe wataenda Yanga. Japo inabidi tujue wenyewe wanasemaje?
0 Comments